1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yatuma vikosi DRC kupambana na waasi

2 Novemba 2022

Rais wa Kenya William Ruto Jumatano alitangaza kutumwa kwa kikosi cha jeshi la nchi yake kwenda mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kushiriki operesheni ya kikanda dhidi ya hujuma zinazoendeshwa na waasi.

https://p.dw.com/p/4IyBT
Somalia Tabda|  Kenianische Soldaten | Militäroffensive
Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Akizungumza katika halfa ya kuwaaga wanajeshi iliyofanyika mjini Nairobi,Rais Ruto amesema kikosi hicho kinakwenda Congo kwa dhima ya "kulinda ubinaadamu" unaowekwa rehani na makundi ya wanamgambo na magaidi wenye silaha.

"Kama majirani wenye nasaba ya pamoja, hatma ya DRC inafungamana na ya kwetu. Sote tuna jukumu katika uthabiti wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na usalama wake ni nadhiri tunayoapa kuitimiza," alisema Ruto.

Kikosi hicho cha Kenya ni sehemu ya ujumbe wa kijeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioidhinishwa na wakuu wa nchi wa kanda hiyo mnamo mwezi April,  kuisaidia Congo kuyashinda makundi ya wapiganaji upande mashariki.