Kenya yataka kujitoa katika mkataba wa Roma
6 Septemba 2013Kura hiyo imepigwa siku chache tu kabla ya kesi dhidi ya Ruto kuanza mjini The Hague, Uholanzi, ikiifanya Kenya kuwa nchi ya kwanza kuitisha kura kama hiyo bungeni.
Hata kama kura hiyo ya aina yake inatoa onyo kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, hata hivyo haina uzito kwa kesi ya viongozi hao wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Bunge la Kenya linabidi lipitishe mswaada huo wa sheria katika kipindi cha siku 30 zijazo ili kuhalalisha hatua za kujitoa katika mkataba wa Roma.
Mswaada wa "kusitisha,aina yoyote ya mshikamano,ushirikiano na msaada" pamoja na mahakama ya ICC umeungwa mkono kwa wingi wa kura.
Jumanne ijayo mahakama ya ICC imepanga kufungua kesi dhidi ya makamo wa rais William Ruto kwa madai ya kufanya uhalifu dhidi ya ubinaadam..Anatuhumiwa kuandaa machafuko ya baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008 yaliyoangamiza maisha ya watu wasiopungua 1100 na kuwalazimisha wengineo zaidi ya laki sita kuyahama maskani yao.
Mbali na Ruto,na rais Kenyatta pia anashitakiwa
Kesi ya Ruto inasadifu miezi kama miwili hivi kabla ya rais Uhuru Kenyatta kufika mahakamani kwa madai ya uhalifu dhidi ya ubinaadam,ikiwa ni pamoja na mauwaji,ubakaji,mateso na kuwalazimisha watu wayahame maskani yao.
Wote wawili,Kenyatta na Ruto,wanaopinga tuhuma dhidi yao,walisema wako tayari kushirikiana kikamilifu na mahakama ya kimataifa ya ICC.
Mwengine anaetarajiwa kufikishwa mahakamani mjini The Hague ni mkuu wa kituo cha Radio Joshua Arap Sang anaetuhumiwa kuchochea matumizi ya nguvu.
Katika mjadala moto moto wa bunge mkuu wa kundi linalodhibiti viti vingi bungeni Aden Duale alisema "kujitoa katika ICC ni kuilinda katiba na kuitakasa hadhi ya Kenya."
Lakini kiongozi wa upande wa upinzani Francis Nyenze amehoji kujitoa katika ICC kutaichafulia Kenya hadhi yake kimataifa.
Wanasiasa wengi wa Kenya wanaiangalia mahakama ya kimataifa ya ICC kuwa ni chombo cha "ukoloni mambo leo" kinachowaandama waafrika tu.
Licha ya uamuzi wa bunge,kesi zitaendelea
Muungano wa Jubilee unaowajumuisha pia Kenyatta na Ruto unathibiti wingi wa viti katika bunge la Kenya na baraza la Seneti ambalo limepanga kulijadili suala hilo hilo wiki ijayo.
Juhudi zozote za kujitoa zitahitaji zipitie katika Umoja wa mataifa utaratibu ambao unaweza kudumu angalao mwaka mmoja."Kujitoa katika ICC hakutaathiri hata kidogo kesi wala mashtaka" amesema msemaji wa ICC Fasdi El Abdallah katika taarifa yake.
Kura ya maoni au uamuzi wa serikali hautabadilisha jukumu la Kenya kushirikiana kikamilifu na ICC kuambatana na sheria za kimataifa.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imeitaka serikali ya Kenya iheshimu kikamilifu ahadi zake za kuhakikisha wahanga wa matumizi ya nguvu ya baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008 wanatendewa haki."
Shirika linalopigania haki za binaadam la Amnesty International limelaani uamuzi wa bunge la Kenya na kuonya uamuzi huo unaweza kuinyima Kenya "kinga muhimu kabisa ya haki za binaadam."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu