1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yasema mikakati ipo kukabiliana na nzige wa jangwani

Shisia Wasilwa10 Januari 2020

Wizara ya kilimo nchini Kenya imewahakikishia wananchi kuwa imeweka mikakati ya kutosha kukabiliana na nzige wa jangwani ambao wamevamia maeneo kadhaa nchini humo.

https://p.dw.com/p/3W0Mu
Somalia Heuschreckenplage Bauern
Picha: Reuters/F. Omar

Serikali ya Kenya imewahakikishia wananchi kuwa imeweka mikakati ya kutosha kukabiliana na nzige wa jangwani ambao wametokea nchi jirani za Ethiopia na Somalia. Nzige hao wameyavamia maeneo ya kaskazini mwa Kenya hivyo kuhatarisha hali ya chakula nchini. Akiwahutubia wanahabari waziri wa kilimo Mwangi Kiunjuri amewataka wananchi kuwa waangalifu na kutoa taarifa kwa mamlaka  kuhusu wadudu hao. 

Wizara ya kilimo imebuni kitengo cha kukabiliana na nzige wa jangwani na kuwaleta wadau wote pamoja ambao watachangia kuleta ufumbuzi wa wadudu hao wanaohama kwa pamoja saa za asubuhi na kupumzika wakati wa mchana. Nzige hao waliripotiwa kuingia nchini tarehe 28 mwezi Desemba mwaka uliopita na kuvamia kaunti za Wajir, Marsabit na Mandera , baada ya kusababisha uharibifu wa mazao katika mataifa ya Somalia na Ethiopia. Serikali ya Kenya inakabiliwa na changamoto ya kuwakabili wadudu hao, kwani makao makuu ya kuwakabili yanapatikana Ethiopia. Hata hivyo waziri wa kilimo nchini Kenya Mwangi Kiunjuri amebuni kamati ya kuwakabili.

Nzige wa jangwani ni waharibifu kwa mimea na majani
Nzige wa jangwani ni waharibifu kwa mimea na majaniPicha: AP

Tayari ekari 175,000 za mashamba katika mataifa ya Somalia na Ethiopia, yameharibiwa na nzige hao katika uvamizi mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya miaka 70, kwa mujibu wa Shirika la Kilimo Ulimwenguni, FAO. Serikali ya Kenya imeweka lita elfu tatu za kemikali za kukabiliana na wadudu hao pamoja na ndege tatu za kunyunyizia dawa.

Shirika hilo la FAO limeonya kuwa huenda nzige hao wakaongezeka hata zaidi kufuatia mvua zinazoendelea kushuhudiwa, kwani ni mazingira mazuri ya kuzaliana. Nzige wa kike ana uweza wa kutaga mayai 300 kwa siku, hivyo kuongeza idadi yao kwa kasi. Hadi kufikia sasa nzige wameripotiwa kushuhudiwa katika kaunti tano, ya Meru ikiwa ya hivi karibuni. Wakulima wa kaunti hiyo wanahofia kuwa mimea yao huenda ikaathiriwa.

Huku wasiwasi wa wadudu hao ukisambaa kama moto jangwani, wanasayansi wanawashauri watu walioathiriwa kuwafanya kitoweo kwani wanasemekana kuwa na  hamirojo ya protini. Jamii ya watu kutoka Magharibi ya Kenya huwala nzige hao baada ya kuwachemsha au kuwakaanga. Serikali ikishirikiana na Shirika la kudhibiti nzige Afrika Mashariki inatumia helikopta kunyunyiza kemikali katika maeneo yaliyoathiriwa.