1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yasema al Shabaab imekita mizizi

Admin.WagnerD9 Oktoba 2013

Ripoti ya shirika la taifa la kijasusi nchini Kenya, NSIS, inaonyesha kuwa shirika hilo linaamini kuwa makundi ya itikadi kali kama vile Al shabab la nchini Somalia yameimarisha mitandao nchini Kenya na kugeuka tishio.

https://p.dw.com/p/19wYE
Wapiganaji wa al Shabaab wakipewa mafunzo ya vita.
Wapiganaji wa al Shabaab wakipewa mafunzo ya vita.Picha: picture-alliance/AP

Maafisa wa usalama wamekuwa wakishutumiwa kushindwa kuepusha mashambulizi ya kigaidi, hususan jinsi walivyoshughulikia shambulizi lililofanywa na Al Shabab katika jengo la maduka la Westgate mjini Nairobi yapata wiki mbili zilizopita ambapo zaidi ya watu 60 waliuawa. Magaidi walilidhibiti jengo hilo kwa siku kadhaa.

Ripoti iliyovujishwa kutoka shirika la kitaifa la kijasusi la Kenya inaonyesha kuwa shirika hilo lilionya mara kadhaa kuhusu kuendelezwa kwa kiasi kikubwa nyendo za al Shabaab nchini humo kwa madhumuni ya kuishambulia nchi hiyo.

Mnamo tarehe 21 mwezi Septemba, siku hiyo hiyo ambayo Westagate ilishambuliwa, shirika la NSIS lilionya kuwa wapiganaji wa al shabab wako mjini Nairobi na wanapanga kufanya mashambulio ya kujitoa muhanga katika siku ambazo hazikufichuliwa wakilenga jengo la Westgate na kanisa la kikatoliki la Holy Family Basilica.

Washukiwa walihafamika

Ripoti hiyo inaendelea kuwataja washukiwa Sheikh Abdiwelli Mohammed,Sheikh Hussein na Sheikh Hassan kuwa wanaaminika kuwa na fulana mbili za kuwekea mabomu ya kujiripua,maguruneti 12 ya kurushwa kwa mikono bunduki mbili aina ya AK 47 na tayari wameshapekua maeneo hayo mawili yaliyolengwa.

Ripoti hiyo inayoonyesha kuwa asasi za kiusalama nchini Kenya zilikuwa zina ufahamu wa njama hizo za mashambulizi na inaendelea kuwataja washukiwa zaidi Sheikh Hassan kwa jina jingine Blackie anayeishi mtaa wa Majengo mjini Nairobi na Omar Ahmed Ali kwa jina jingine Jerry anayeishi eneo la Huruma katika barabara ya Juja.

Katika ripoti nyingine ya kijasusi kutoka shrika hilo iliyotolewa kwa asasi husika za kiusalama nchini humo, inayoonyesha ilitolewa tarehe moja mwezi Februari mwaka huu, inadokeza kuwa mnamo mwezi Desemba mwaka jana, Al Shabab ilikuwa ikiwafunza wapiganaji wa kike ili kushiriki katika mashambulizi ya kuteka nyara ndege na kuziangusha pamoja na mashambulizi ya kujitoa muhanga.

Inaaminika baada ya mafunzo hayo, wapiganaji hao wa kike walikuwa wapelekwe nchi za magharibi na nchi za Afrika ambazo zilituma wanajeshi wake katika kikosi cha umoja wa Afrika cha AMISOM kupigana nchini Somalia.

Mafunzo ya itikadi kali za kidini

Ripoti iliyotolewa tarehe 25 mwezi Juni mwaka huu ilionyesha kuwa vijana bado wanaendelea kupokea mafunzo ya kidini ya itikadi kali hasa mijini Mombasa na Nairobi. Mjini Mombasa Sheikh Ibrahim Ismael Amru amekuwa akitoa mihadhara katika msikiti wa Minaa mtaani Kisauni akiwahimiza waisalmu kuunga mkono jihad. Watu wasiojulikana waliokuwa na silaha walimuua mhubiri huyo sheikh Ibrahim mwishoni mwa wiki iliyopita.

Na sio hayo tu mnamo tarehe 26 mwezi Agosti, ripoti hiyo ya kijasusi ilionya kuwa washambuliaji wa al Shabaab wanapanga kuyashambulia majengo yenye shughuli nyingi mjini Nairobi ya Times Tower na Nyayo katika tarehe zisizojulikana. Inaaminika kuwa wananuia kutumia mitambo iliyosheheni viripuzi kufanya mashambulizi hayo.

Kufuati ongezeko hilo la vitisho vya mashambulizi yanayopangwa na al Shabaab, mwezi uliopita asasi mbalimbali zilifahamishwa kuhusiana na ongezeko la uwezekano wa mashambulizi zikiwemo wizara ya usalama, fedha, usalama wa ndani, wizara ya mambo ya nje na ofisi ya mkuu wa majeshi nchini Kenya.

Asasi hizi zilionywa kuwa makundi ya kigaidi huenda yakaishambulia Kenya kati ya tarehe 13 na 20 mwezi Septemba, mwezi ambao jengo la Westagate lilishambuliwa.

Mwandishi:Caro Robi/ap

Mhariri:Yusuf Saumu