Kenya yarekodi vifo zaidi kutokana na ajali za barabarani
23 Desemba 2020Mutyambai amewataka watumiaji wa barabara msimu huu wa sikukuu ya Krismasi wawe waangalifu ili kuepusha ajali.
Shamrashamra za sikukuu ya Krismasi zinapowadia, Inspekta Mkuu wa Polisi nchini Kenya, Hillary Mutyambai amesema kuwa vifo vingi vilivyoshuhudiwa mwaka huu vilitokana na watembea kwa miguu.
Ili kuhakikisha kuwa ajali zinapungua kabla ya mwaka kukamilika pamoja na usalama kuimarishwa, Mutyambai amesema kuwa idara yake itawatuma maafisa wake kote nchini. Juma lililopita Mutyambai aliwataka maafisa wake waliokuwa likizo kurejea kazini.
Makosa madogomadogo huchangia pakubwa ajali
"Tathmini ya vyanzo vingi vya ajali vinaonesha kuwa makosa madogo madogo ya uvunjifu wa sheria za barabarani kama vile ulevi na kuzidisha idadi ya watu yamechangia idadi kubwa ya ajali.” Amesema Mutyambai.
Akiwahutubia wanahabari Mutyambai pia alisema kuwa maafisa wa polisi wamepewa amri ya kuhakikisha kuwa masharti ya kukabiliana na virusi vya corona yanazingatiwa.
Mutyambai alikuwa ameandamana na maafisa wa Mamlaka ya Taifa ya Usalama na Uchukuzi-NTSA. Msako wa magari mabovu na yale yanayozidisha kasi ya mwendo iliyokwekwa barabarani umeanza kutekelezwa huku wakosaji wakionywa kuchukuliwa hatua za sheria.
"Tumegundua kuwa kuna utovu wa nidhama kwa watumiaji wa barabara ndio maana unaona ongezeko la ajali za barabarani kwa wanaotembea kwa miguu.” Amefafanua mwenyekiti wa NTSA George Njao.
Ajali zaongezeka licha ya masharti kukabili virusi vya Corona
Ongezeko la vifo barabarani linajiri wakati uchukuzi umepungua kutokana na uzingatiaji wa masharti ya kukabiliana na virusi vya corona huku watu wengi wakifanyia kazi majumbani.
Kwa mara ya kwanza wakati huu maafisa wa magereza watashirikiana na maafisa wengine wa usalama kudumisha usalama nchini na pia kuhakikisha kuwa sikukuu ya Krismasi imesherehekewa bila ya uvunjifu wa sheria.
"Nimeagiza maafisa 5000 wa magereza kusaidia kama maafisa maalum chini ya Inspekta Mkuu.” Amesema Wycliff Ogola, ambaye ni mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Magereza.
Watu 2,492 waliripotiwa kuaga dunia kwenye ajali za barabarani mwaka uliopita. Baadhi ya sababu zilizotolewa za kuongezeka kwa ajali za hizo mwaka huu ni pamoja na uchovu, mwendo kasi, uvunjifu wa sheria za barabarani miongoni mwa sababu nyingine.