Kenya yaomboleza kifo cha mwanariadha Kelvin Kiptum
12 Februari 2024Mwanariadha huyo na kocha wake Gervais Hakizimana wamefariki dunia jana katika ajali ya barabarani iliyotokea eneo la bonde la ufa.
Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ameandika kwenye ukurusa wake wa kijamii wa X kuwa, amesikitika kumpoteza mwanariadha huyo aliyemtaja kama shujaa wa kweli.
Waziri wa michezo wa Kenya Ababu Namwamba pia amehuzunishwa na kifo cha Kiptum.
"Ni asubuhi ya giza, siku ya giza kwa nchi yetu. Siku ya giza kwa ulimwengu wa riadha, nchini Kenya na kote duniani. Tumeishiwa na maneno, kwa kumpoteza kijana mwenye kipaji ambaye ametamba katika ulingo wa riadha duniani akiwa na umri wa miaka 24 tu, na ambaye mustakabali wake katika riadha ulikuwa mzuri na angetawala mbio za marathon kwa muda mrefu," amesema Namwamba.
Soma pia: Mwanariadha Kipyegon wa Kenya ashinda mbio za mita 1500
Rais wa chama cha riadha duniani Sebastian Coe kupitia taarifa yake amesema wameshtushwa na kuhuzunishwa sana na kifo cha Kelvin Kiptum pamoja na kocha wake, raia wa Rwanda Gervais Hakizimana.
Ametoa salamu za rambi rambi akisema wamempoteza mwanariadha mahiri aliyeacha sifa kubwa.
Kelvin Kiptum aliweka rekodi ya dunia katika mashindano ya riadha ya mbio za Marathon ya Chicago mwezi Oktoba kwa kukimbia kwa muda wa saa mbili na sekunde 35 na kuvunja rekodi iliyowekwa na Eliud Kipchoge mjini Berlin mwaka 2022 baada ya kukimbia kwa saa mbili, dakika moja na sekunde tisa.