Kenya yalaumiwa kwa dhuluma dhidi ya jamii ya Sengwer
17 Januari 2018Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya yamelaani vikali hatua ya serikali ya kuwaondoa kwa nguvu watu wa jamii ya Sengwer wanaoishi kwenye msitu na kusababisha kifo cha mtu mmoja. Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Amnesty International Houghton Irungu ameitaka serikali kuzingatia haki za binadamu inapotekeleza hatua ya kuwaondoa watu hao. Hata hivyo jamii hiyo sasa inasema kuwa mradi unaotekelezwa na Jumuiya ya Ulaya wa kuhifadhi mazingira usitishwe kwani hayo ni makazi yao tangu kale.
Jamii ya Sengwer imekuwa ikipinga vikali hatua ya kuhamishwa kwenye msitu wa Embobut tangu mwaka 2007 ikisema kuwa eneo hilo ni ardhi yao ya ukoo. Msitu wa Emobut ni moja ya vyanzo vya maji nchini Kenya. Jumuiya ya Ulaya inatekeleza mradi wa maji unaogharimu shilingi bilioni 3.6 unaolenga kuhifadhi maji na kuuinda msitu huo. viongozi wa jamii hiyo wanasema kuwa hawakushauriwa wakati mradi huo ulipokuwa unatekelezwa.
Serikali ifuate katiba inapowahamisha watu
Shirika la kitaifa la kutetea haki za binadamu limesema kuwa serikali inastahili kuzingatia katiba inapowahamisha wakazi wa jamii hiyo kwani uharibifu wa mali yao nawakati mwengine utumiaji wa nguvu kupita kiasi ni kinyume cha sheria. Houghton Irungu amesema:
“Tunazo picha za watu waliouawa hatutazionesha kwasababu ya heshima kwa familia lakini zinaonesha wazi kile kilichofanyika katika muda wa saa 24 zilizopita.”
Miongoni mwa wito ambao jamii hiyo inatoa sasa, ni kusitishwa kwa mradi huo na kusitisha mipango ya mashirika yote yanayofadhili mpango huo likiwemo shirika la huduma za misitu nchini ambalo limekuwa likitumika kuwaondoa bila ya kuzingatia haki za binadamu. Jumanne iliyopita, mmoja wa viongozi wa jamii hiyo alipigwa risasi na walinzi wa misitu. Licha ya kunusurika, nyumba yake iliteketezwa na mali yake kuharibiwa.
Serikali ya Kenya pia ilikiuka haki za jamii ya Ogiek
Mwezi Mei mwaka uliopita, mahakama ya Afrika inayoshughulikia haki za binadamu ilibaini kuwa serikali ya Kenya ilikiuka haki za jamii ya Ogiek inayoishi kwenye msitu wa Mau ilipokuwa inawaondoa. Sengwer ni moja ya watu ambao wangali wanaishi msituni nchini Kenya. Hayo yanajiri siku moja baada ya wataalamu watatu wa Umoja wa Mataifa kueelezea wasiwasi wao kuhusu ripoti za hivi karibuni kuhusu mashambulio dhidi ya jamii ya Sengwer.
Wataalamu hao John Knox, Michel Forst, na Victoria Tauli-Corpuz, ni wataalam wa masuala ya haki za jamii za wakaazi asili Kwenye taarifa yao ya pamoja, watatu hao wameihimiza serikali kuhakikisha kuwa haki za watu wa jamii ya Sengwer zimeheshimiwa, licha ya kuwa mradi wa Jumuiya ya Ulaya wa kuhifadhi maji na tabia nchi unatekelezwa.
Tarehe 25 mwezi Desemba mwaka uliopita, zaidi ya wahudumu 100 wa kulinda misitu waliokuwa na bunduki walivamia msitu wa Embobut wanakoishi wasengwer na kuteketeza nyumba zao na kuua mifugo yao.
Mwandishi: Shisia Wasilwa, DW, Nairobi
Mhariri: Yusuf Saumu