1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yakosolewa kwa kuwarejesha kwao Wasomali

Josephat Nyiro Charo23 Mei 2014

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti leo likisema Kenya imewarudisha kwao Wasomali 359, wakiwemo wakimbizi wapatao 3, tangu ilipoanza operesheni ya usalama mapema Aprili 2014.

https://p.dw.com/p/1C5Pd
Kenia Dadaab, Somalische Flüchtlinge
Picha: Getty Images

Katika ripoti hiyo Kenya imenyooshewa kidole cha lawama kwa kukataa kumruhusu mtu yeyote kupinga kurejeshwa kwa Wasomali nchini kwao kwenye vita na machafuko. Katika hatua ya hivi karibuni Kenya imewarudisha Wasomali 98, wakiwemo watoto 12 mjini Mogadishu Mei 20 bila kulionya shirika linalowahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, kuhusu hatua hiyo.

"Kuwarejesha watu katika maeneo ya vita nchini Somalia kunaonyesha hali ya kutojali kabisa haki zao na usalama wao," amesema Gerry Simpson, Mtafiti mwandamizi wa shirika la Human Rights Watch. "Heshima ndogo iliyosalia kwa Kenya kutambua na kuheshimu haki za kimsingi za wakimbizi inapotea kwa kasi kubwa," akaongeza kuongeza mtafiti huyo.

Kwa mujibu wa shirika la UNHCR Kenya iliwarejeresha Wasomali 91 mnamo Aprili 17 na wengine 87 Mei 3. Shirika hilo limesema maafisa wa Kenya walilizuia kuyafikia makundi matatu ya Wasomali waliorudishwa kwao kabla kuondolewa kutoka Kenya. Laetitia Bader, Mtafiti wa shirika la Human Rights Watch mjini Nairobi, Kenya anasema, "Umoja wa Mataifa unatakiwa kutekeleza mamlaka yake ya ulinzi. UNHCR inahitaji kuwafikia watu wanaozuiliwa katika vituo vya polisi mjini Nairobi na sehemu nyingine za Kenya, lakini hasa watu wanaokabiliwa na hatari ya kurejeshwa kwao."

Gerry Simpson
Gerry Simpson, Mtafiti wa Human Rights WatchPicha: 2013 Byba Sepitkova/Human Rights Watch

Kenya yatakiwa kuiruhusu UNHCR iingilie kati

Shirika la Human Rights Watch limesema serikali ya Kenya inapaswa iwaruhusu Wasomali waliotambuliwa na kuorodheshwa kwa ajli ya kurejeshwa kwao wapinge hatua hiyo mahakamani au waombe uhifadhi na idara husika au shirika linalowahudhumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR. Shirika la UNHCR linatakiwa liruhusiwe bila pingamizi zozote kumfikia Msomali yeyote aliyetambuliwa kwa lengo la kurudishwa Somalia.

Laetitia Bader wa shirika la Human Rights Watch amesema, "Tumekuwa tukiwasiliana na serikali ya Kenya kuhusu suala hili. Ni tatizo kubwa jinsi polisi wanavyofanya kazi yao na tumeelezea wasiwasi wetu na malalamiko yetu."

Kenya iliacha kuwasajili watu waliomba uhamiaji mijini mnamo Desemba mwaka 2012. Kwa mantiki hiyo Wasomali wanaowasili jijini Niarobi na miji mingine tangu wakati huo hawajafaulu kupata vibali vya uhamiaji.

Mtafiti wa Human Rights Watch Gery Simson amesema kama Kenya haitaki kutimiza majukumu yake ya kitaifa na kimataifa ya kisheria na kuwasajili watu wanaoomba hifadhi na kuyashughulikia maombi yao kabla kuwarejesha, inatakiwa iliruhusu shirika la UNHCR liingilie kati kufanya hivyo.

Mwandishi: Josephat Charo/Human Rights Watch

Mhariri: Mohammed Khelef