1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yajiweka tayari kwa kesi za uchaguzi

Thelma Mwadzaya17 Agosti 2022

Wanasiasa wa muungano wa Kenya Kwanza ulio chini ya rais mteule wa Kenya William Ruto wanakutana leo Jumatano (17.08.2022) na washindi wao wa uchaguzi.

https://p.dw.com/p/4Fd68

Muungano wa Kenya Kwanza unawaleta pamoja washindi wake wa uchaguzi mkuu ulopita kwenye makaazi rasmi ya rais mteule William Ruto yaliyoko mtaani Karen. Kikao hicho kimepangwa kuanza saa tatu asubuhi. 

Kwenye taarifa yake ya Jumanne, Katibu Mkuu Veronica Maina, alifafanua kuwa mkutano huo utawaleta pamoja Maseneta, Wabunge na Magavana wateule.

Wawakilishi wa wadi wataandaliwa kikao tofauti katika siku zijazo.

Kwa upande mwengine, mgombea wa urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, yumkini anajiandaa kuelekea kwenye mahakama ya juu kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyomnyima ushindi.

Akizungumza kwenye ukumbi wa mikutano wa KICC, Raila alisisitiza kuwa atachukua hatua zote za kisheria ili matokeo ya uchaguzi yawe batili.

Alimlaumu mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Wafula Chebukati kwa kutangaza matokeo hayo kimabavu na kuwatenga makamishna wake.

Mahakama yajitayarisha kupokea mashauri ya uchaguzi 

Kenia Nairobi | Raila Odinga und Unterstützer
Raila Odinga yumkini atayapinga matokeo mahakamani Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Wakati huohuo, Mahakama ya Juu inakamilisha maandalizi ya kupokea kesi za uchaguzi endapo zitawasilishwa. Kufikia Jumanne wiki hii,ukumbi mkuu kwenye Mahakama ya Milimani iliyoko mtaani Upperhill hapa jijini Nairobi, ulikuwa umeandaliwa.

Viti vitakavyotumiwa na mawakili na wateja wao vilikuwa vimeshapangwa. Ukumbi huo una viti 40 vya umma pamoja na majaji 7 wa Mahakama ya Juu.

Kwa mara ya kwanza vikao vya mahakama ya juu vitahamishwa kutokea majengo ya katikati ya jiji hadi Upperhill.

Inasadikika kuwa azma ya hatua hiyo ni kuepusha msongamano. Walalamikaji wamepewa siku saba hadi Jumatatu ijayo kuwasilisha kesi kwenye eneo la usajili la jengo la Forodha kwenye mahakama kuu ya Milimani.

Kifo cha afisa wa Tume ya Uchaguzi chaanza kuchunguzwa 

Kenia | Ein kenianisches Gangmitglied hält eine Machete fest
Picha: DW

Yote hayo yakiendelea, mwendesha mashtaka mkuu nchini Kenya Noordin Haji amethibitisha kuwa anafuatilia kwa karibu uchunguzi wa kifo cha afisa msimamizi wa IEBC Daniel Musyoka aliyepotea Alhamisi iliyopita na maiti yake kupatikana Jumatatu wiki hii.

Daniel Musyoka alitoweka Alhamisi iliyopita alipokuwa kwenye majukumu yake ya kazi katika kituo cha kuhesabia kura cha Embakasi East.

Maiti yake ilipatikana kaunti ya Kajiado na walisha wa mifugo walioiarifu idara ya polisi.Familia yake tayari imefika kuthibitisha maiti inayohifadhiwa kwenye hospitali ya Loitoktok.

Kwa upande mwengine, Baraza Kuu la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali linamrai rais mteule William Ruto kumnyoshea mkono wa amani na upatanishi mtangulizi wake Uhuru Kenyatta.

Akizungumza na waandishi wa habari, mwenyekiti wa baraza hilo, Stephen Cheboi, aliusisitizia umuhimu wa viongozi hao watatu kukaa pamoja kwenye meza ya mazungumzo kwa manufaa ya taifa.

Ifahamike kuwa hakuna matokeo ya uchaguzi wa rais ambayo hayajapingwa tangu mwaka 2002. Azimio la Umoja One Kenya nao pia wanajiandaa kukutana na washindi wao wa uchaguzi mkuu kwenye ukumbi wa KICC.