Kenya: Wakaazi wataka kuunganishiwa huduma ya umeme
27 Septemba 2023Jimbo hilo linakaliwa na kampuni kubwa zaidi ya kuzalisha nishati kutumia upepo barani Afrika ila serikali haijawaunganisha kupata umeme huo.
Tatizo la kukatika kwa umemelimekuwa ni jambo la kawaida katika mjini wa Marsabit kwa muda mrefu na wakaazi wengi wamekuwa wakilazimika kutumia mitambo ya jenereta na nishati jadidifu ikiwemo umeme wa kawi kuendesha shughuli zao za kijamii na kiuchumi.
Hali hiyo imekuwa ni kadhia kwa muda mrefu kwa wakaazi wa eneo hilo ambao kwa wakati huu wameingia barabarani wakiwa wamebeba mabango yanayoelezea kero zao.
Soma pia:Mfumuko wa bei, kodi na maandamano: Mwaka mgumu wa kwanza kwa Ruto
Mamia ya wakaazi wanaishinikiza serikali kupitia wizara ya nishati nchini kuwapa mgao wao wa umeme kupitia gridi ya kitaifa kutokana na kwamba,jimbo hilo linazalisha nishati ambayo inatumika sehemu nyingine za taifa.
Serikali ya Kenya haijachukua hatua
Kulingana na mwenyekiti wa kamati ya ardhi na umeme katika bunge la kaunti ya Marsabit Jacob Elisha, juhudi zao za kutafuta suluhu la kudumu limeshindikana kutokana na ahadi za kila mara kutoka kwa serikali.
''Tumejaribu kufuatilia kupitia kampuni ya Kenya Power,lakini hakuna mafanikio"
Alisema licha ya kwenda kwenye ofisi za serikali zinazohusika na masuala ya nishati lakini hakuna jitihada zilizofua dafu.
"Wananchi wa Marsabit hawana stima kwa miaka mitano sasa.'' Alisisitiza.
Mwaka wa 2018, kampuni ya Ziwa Turkana inayozalisha nishati ya umeme kwa kutumia upepo, ilianza kutuma umeme kwa gridi ya taifa eneo la Suswa ila hadi leo, wakaazi wa Marsabit hawajaunganishwa na umeme huo.
Soma pia:Kenya yahitimisha siku ya tatu ya maandamano
Maandamano ya leo yanafungua ukarasa mpya kwa wakaazi wa Marsabit kupata mgao wa umeme kutoka gridi ya kitaifa.
Wakaazi hao wamesisitiza kuendelea na maandamano hayo hadi serikali itakapowaunganisha na umeme wa kitaifa.
Wananchi wa Marsabit wanasema wamesahaulika na mamalaka kwa masuala ya umeme na wamesema wataendelea kusalia mitaani hadi kero hiyo itapotatuliwa.