Kenya: Viongozi wa dini wagawanyika kuhusu mageuzi ya katiba
2 Septemba 2020Mitazamo tofauti na mikali imetawala kati ya viongozi wa kidini na makanisa mintarafu mageuzi ya katiba. Hali hiyo inaaminika kuwa inaweza kuwachanganya wafuasi wa dini na madhehebu mbalimbali.
Kwa upande wake Baraza kuu la Waislamu nchini Kenya linaunga mkono mageuzi ya katiba ila suala la iwapo muda ni sahihi limejitokeza. AbdiLatiff Shaban ni mkurugenzi mkuu wa baraza kuu la waislamu nchini Kenya na huu ndio mtazamo wake.
"Kwakweli hiyo haja ipo, pengine swala la kujiuliza ni kwanini sasa? kwanini sio mwaka ujao?kwanini sio baada ya uchaguzi tunaoutarajia mwaka 2022?. Ingekuwa vizuri haya maswali tungeweza kuyazungumzia"
Kwa upande mwengine, Kanisa Katoliki nchini Kenya limeashiria kuwa huenda likaipinga kura ya maoni kwani inaweza kuleta migawanyiko, kuwa na gharama nyingi kadhalika ubadhirifu. Kwa mujibu wa taarifa ya Muungano wa maaskofu wa kikatoliki nchini Kenya iliyotolewa mwanzoni mwa wiki, mapendekezo yoyote ambayo yatakuwa ya muda mfupi na hayawakilishi matakwa ya wengi lazima yakataliwe. Wakati huo huo, kanisa la Kianglikana la Kenya lililo na sauti kubwa kuhusu mageuzi linakiri kuwa muda umewadia kuifanyia katiba mageuzi.
Askofu mkuu Jackson Ole Sapit wa kanisa la kianglikana alifafanua kuwa muda umewasili kuitazama upya katiba ya nchi na kuifanyia kazi. Askofu mkuu Sapit aliwarai wakenya kutokuwa na hofu kuhusu kura ya maoni kwa misingi ya vurugu kuzuka. Badala yake mchakato huo utajikita kwenye kuyafanyia kazi mapungufu ya katiba ya 2010.
Baraza kuu la makanisa limetoa ishara kuwa huenda likaunga mkono kura ya maoni ila mchakato huo lazima ujikite kwenye kuwapa kipaumbele wakenya wenyewe na mahitaji yao. Wakati huo huo makanisa ya Protestanti, kupitia taarifa yao, yanashauri kura ya maoni kufanyika iwapo itawaleta wakenya pamoja.
Taarifa hiyo ilitiwa saini na katibu mkuu Canon Chris Kinyanjui na mwenyekiti wa baraza la makanisa ya Kiprotestanti Askofu Mkuu Timothy Ndambuki. Baraza kuu la makanisa la Kenya linataka mageuzi yatakayoandaa jukwaa la kuunda serikali itakayowashirikisha wote na kuupa nguvu na sauti upinzani. Soma Mchakato wa marekebisho ya katiba Kenya waanza
Kwa upande mwengine mwenyekiti wa zamani wa muungano wa makanisa ya Kiinjili Askofu Mark Kariuki aliyepia mkuu wa kanisa la Deliverance nchini Kenya, ametahadharisha kuhusu kuipanua serikali kwani gharama hizo zitamuumiza mwananchi wa kawaida. Endapo hilo litakuwa lengo la mageuzi basi kanisa halitakuwa na budi kuipinga kura ya maoni.
Itakumbukwa kuwa mwaka 2010 makanisa yalimuunga mkono naibu wa rais William Ruto aliyekuwa upande wa kupinga mageuzi ya katiba kwa msingi kuwa baadhi ya mambo yaliwakera kama uavyaji wa mimba. Kwa sasa hali haitabiriki ijapokuwa msimamo wa naibu wa rais William Ruto ni kuyalinda maslahi ya wakenya.
Siku chache zilizopita Rais Uhuru Kenyatta kwenye hotuba yake kwa taifa aliusisitizia umuhimu wa kuandaa hati ambayo itawanufaisha wakenya kwani muda umewadia kuitathmini upya katiba.
Thelma Mwadzaya, Nairobi.