Kenya: Televisheni zaacha kuchapisha matokeo ya urais
12 Agosti 2022Wachambuzi na waandishi wa habari nchini Kenya wameshituka na kuelezea wasiwasi wao, baada ya kugundua kuwa vituo vya televisheni vya KTN, NTV na Citizen vimepunguza kasi au kusimamisha kabisa mchakato wa kuchapisha matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais, kadri yanavyoingia.
Soma zaidi: IEBC haijamaliza kutangaza matokeo siku tatu baada ya uchaguzi
Hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa na vituo hivyo juu ya sababu ya kusitisha ghafla uchapishaji huo wa matokeo ya mwanzo, kulikofuatia hakikisho la mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya, IEBC Wafula Chebukati kwa raia, akiwataka kutohofu chochote kutokana na matokeo yasiyofanana yaliyokuwa yakitolewa na vyomba vya habari.
Matokeo yasiyofanana yalikuwa yanaanza kuzua mashaka
Hata kabla ya hatua hiyo, mashaka yalikuwa yameibuka miongoni mwa Wakenya, kufuatia vituo hivyo kuchapisha matokeo ya awali yanayokinzana, katika kinyang'anyiro hicho ambapo mgombea wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga anachuana vikali na Naibu Rais William Ruto anayepeperusha bendera ya muungano wa Kenya Kwanza.
Soma zaidi: Baraza la Habari Kenya na hofu ya upotoshaji wa matokeo
Hadi sasa, zoezi hilo la uchaguzi wa Jumanne limekuwa likiendelea kwa amani, tofauti na chaguzi za miaka ya nyuma ambazo ziliambatana na visa vya ghasia, ambavyo wakati mwingine vilihusisha umwagaji wa damu.
Akizungumza na shirika la habari la Associated Press leo Ijumaa, David Omwoyo, mkurugenzi mkuu wa Baraza la Habari la Kenya ambalo liliundwa na serikali, amesema baraza hilo halijakiamuru chombo chochote cha habari kuacha kutoa matokeo. Hata hivyo, ameongeza kuwa baraza lake limetaka uwepo uwiano katika matokeo yanayotangazwa na vyombo hivyo. Omwoyo amesema alikuwa njia kuelekea kwenye mkutano na viongozi wa mashirika ya habari.
Tuhuma za uchakachuaji zaanza kujitokeza
Mashaka ya Wakenya yaliongezeka baada ya jana usiku Katibu mkuu wa chama tawala, kutamka bila kutoa ushahidi wowote kuwa uchaguzi wa rais ulikuwa umekumbwa na udanganyifu mkubwa.
Katika taarifa yakec, afisa huyo mwandamizi wa chama cha Jubilee alisema vimekuwepo vitisho dhidi ya wapigakura, rushwa na kuonyesha kinyume cha sheria vifaa vya uchaguzi katika vituo vya kupigia kura, unyanyasaji dhidi ya mawakala wa vyama katika vituo hivyo, na kutumia visivyo vifaa vya kielektroniki.
Soma zaidi: Kenya yadhamiria kudhibiti vurugu za uchaguzi
Tume ya IEBC ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza matokeo ya mwisho, lakini ilikuwa imeviruhusu vyombo vya habari kujumlisha matokeo na kuyatangaza kadri yanavyoidhinishwa kutoka vituoni.
-rtre, ape, afpe