1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya nayo yaingia taharuki ya kirusi cha corona

16 Machi 2020

Hofu imetanda nchini Kenya baada ya watu wengine wawili kutangazwa kuwa wameambukizwa virusi vya corona, huku shule na taasisi zote za elimu zikifungwa kuanzia Jumatatu sambamba na marufuku nyengine kadhaa.

https://p.dw.com/p/3ZVOq
Kenia Coronavirus Uhuru Kenyatta
Picha: PSCU

Shughuli katika jiji la Nairobi ziliripotiwa kuathirika pakubwa siku ya Jumatatu (16 Machi) huku watu wengi wakiamua kusalia majumbani mwao, baada ya agizo la Rais Uhuru Kenyatta kuwa hatua hiyo itapunguza maambukizi ya virusi hivyo.

Misongamano ambayo hushuhudiwa katika vituo vya mabasi imepungua kwa kiasi kikubwa.

Watu hao wawili walioambukizwa inaaminika kuwa walikaribiana na mgonjwa aliyegunduliwa na ugonjwa huo kwa mara ya kwanza ambaye alitokea Marekani tarehe 5 Machi, na kuingia nchini Kenya. Watu hao ni miongoni mwa wengine 27 waliowekwa kwenye karantini siku ya Jumamosi.

Serikali imesitisha safari zote, hususan kwa watu wanaotokea mataifa yaliyoathiriwa na virusi hivyo.

Wafanyabiashara wakaidi marufuku ya Rais Kenyatta?

Hata hivyo, baadhi ya wafanyiabiashara wamefika jijini Nairobi, licha ya rais kutoa agizo kwa watu kubakia nyumbani. 

Kwenye maduka ya jumla, foleni ndefu zimeonekana za watu wanaowania kununua bidhaa za msingi, huku baadhi ya wauzaji wakiongeza maradufu bei ya bidhaa.

Kenia Coronavirus  Uhuru Kenyatta Meeting
Rais Uhuru Kenyatta akiongoza kikao cha majadiliano kuhusu njia za kukabiliana na virusi vya corona.Picha: PSCU

Ili kuulinda umma kutokana na wafanyabiashara madhalimu, Rais Kenyatta ambaye amelazimika kufuta safari yake ya Vatican, nchini Italia, alisema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watu watakaopatikana wakitumia janga hilo kuficha bidhaa au kuongeza bei ya bidhaa hizo.

Mahakama nayo yaathirika

Mripuko wa virusi hivyo umeathiri sio tu sekta ya uchumi lakini pia idara ya mahakama. Idara hiyo sasa imetangaza kuwa inapunguza shughuli zake kwa kipindi cha majuma mawili yajayo kuanzia Jumatatu.

Wafungwa pamoja na wale walioko kwenye rumande hawataruhusiwa kuelekea mahakamani kwa majuma hayo ili kuweka mikakati mwafaka ya kukabiliana na virusi vya corona, kwa mujibu wa Jaji David Maranga. 

"Watu wote watakaotiwa nguvuni, isipokuwa wale wenye kesi nzito, watashughulikiwa kwenye vituo vya polisi kwa mujibu wa utaratibu utakaotolea na Inspekta Mkuu wa Polisi,"alisema rais huyo wa Idara ya Mahakama.

Watu wamehimizwa kutumia simu na kadi kununua badala ya kukamata pesa ili kupunguza maambukizi ya virusi hivyo katika kipindi hiki, kuepuka mikusanyiko na kunawa mikono kwa kutumia sabuni.

Kwa sasa, Kenya ina visa vitatu vilivyothibitishwa vya virusi vya corona, lakini tayari ni mtihani mkubwa kwa sekta ya afya ambayo imeonekana kukabiliwa na changamoto nyingi. 
 

Shisia Wasilwa, DW Nairobi