Kenya na Somalia zavutana juu ya mpaka wa baharini
16 Septemba 2016Eneo dogo la pembe tatu katika pwani ya Bahari ya Hindi lenye takribani ukubwa wa kilomita 100,000 za mraba ndicho chanzo cha mgogoro baina ya nchi mbili jirani, Kenya na Somalia.
Kila upande unataka sehemu hiyo kwa sababu ya rasilimali za mafuta na gesi zilizogundulika katika eneo hilo, lakini bado haijafahamika ni nani hasa mwenye haki ya kumiliki sehemu hiyo.
Bwana Timothy Walter kutoka Chuo cha Utafiti wa Masuala ya Usalama juu ya Migogoro ya Mipaka ya baharini cha Afrika Kusini (ISS) anasema hali ya mpakani baina ya nchi hizo mbili ni ya mashaka.
Mwaka 2009, nchi hizo mbili zilikubaliana kufanya mazungumzo chini ya Tume ya Usuluhishi ya Umoja wa Mataifa juu ya kulitatua tatizo hilo na kuepuka kulipeleka mahakamani, lakini hilo halikuwezekana.
Kwa jinsi mpaka ulivyo, inaeleweka kwa upande wa Kenya kwa sababu nchi hiyo ina sehemu kubwa na tayari imeshauza leseni kwa makampuni ya kimataifa ya mafuta, ila Somalia haikubaliani na hatua hiyo.
Athari kwa mataifa jirani
Matakwa ya Kenya juu ya mpaka wake na Somalia yamebadilika kwa kiwango kikubwa, anasema Bwana Walter, na "ikiwa mahakama itaipa haki Somalia, hatua hiyo itasababisha mgogoro mkubwa baina ya Kenya na nchi jirani ya Tanzania, mgogoro huo unaweza kuziathiri pia Msumbiji, Madagascar na Afrika Kusini."
Kwa jumla, wataalamu wanafuatilia kwa umakini migogoro inayotokea katika mipaka ya baharini na hasa barani Afrika. Nchi nyingi za Afrika hazina walinzi wa pwani au majeshi ya majini, hata hivyo nchi hizo zinazidi kutambua umuhimu wa rasilimali za baharini kutokana na teknolojia za kisasa. Kwa ajili hiyo, nchi hizo zinahitaji mipaka rasmi, kwa mujibu wa Bwana Walter.
Magharibi mwa bara hilo, mataifa ya Ghana na Cote d'Ivoire nayo yana mzozo kama huo kuhusiana na mpaka kwenye Bahari ya Atlantiki. Kwa sasa mataifa yote mawili yanasubiri hukumu ya Baraza la Upatanishi juu ya Haki za Bahari, ambalo ni mbadala wa Mahakama ya Kimataifa.
Wakati huo huo, taifa la Malawi lililoko kusini mashariki mwa Afrika linalumbana na Tanzania juu ya umiliki wa Ziwa Tanganyika na inafahamika kuwa chimbuko la mzozo huo ni uwezekano wa kuwepo nishati ya mafuta kwenye eneo hilo.
Mwandishi: Friedrike Müller-Jung
Tafsiri: Zainab Aziz
Mhariri: Saumu Yussuf