Kenya: Mzozo wafukuta kuhusu msitu wa Mau
4 Septemba 2019Chama cha kitaifa cha mawakili nchini Kenya, LSK, kimewasilisha ombi la kutaka wajumuishwe kwenye kesi inayohusu mpango wa serikali kuwafurusha watu kutoka msitu wa Mau.
Ingawa wanaunga mkono mpango wa serikali wa kuuhifadhi msitu huo, wanasema wanataka kuisaidia mahakama kuelewa sera na sheria zinazohusu mazingira, ardhi na haki za kibinadamu.
Wakili Kipng'eno Ngetich mwanachama wa LSK ameshauri zoezi la kuwafurusha watu lisitishwe ili kutoa nafasi kwa swala hili kushughulikiwa kisheria na ndiyo maana wameenda mahakamani kutaka muongozo wa kisheria.
Katika awamu hii ya pili serikali inapanga kuziondoa takriban familia elfu 60 kutoka msitu Mau lakini mchakato huo umeibua vuta ni kuvute wengi wa wakaazi wa eneo hili wakisisitiza wana hati halali za umiliki wa ardhi wanamoishi.
Maelewano hakuna
Kiongozi wa maseneta walio wengi katika bunge la seneti Kipchumba Murkomen amemkosoa waziri wa ardhi Keriako Tobiko kwa kuyakaidi mamlaka ya rais na kuwalazimishia ajenda yake anayosema sio halali. Murkomen anadai baraza la mawaziri halijapitisha maafikiano hayo.
Tayari baadhi ya watu wameshaanza kuondoka kutoka maakazi yao huko msitu Mau huku serikali ikiwapa muda wa siku 60 kuondoka kwa hiari kuepuka kuondolewa kwa nguvu makataa hiyo itakapoisha.
Wakili Kipng'eno Ngetich vilevile anahoji kuwa maeneo ya Narok yanayoangaziwa huenda iwe ardhi ya ujumla ya jamii na ipo haja ya kuwahusisha wasoroveya kutoa mwelekeo hususan. Anashauri zoezi hilo lifanywe kwa kuzishirikisha asasi zote zinazohusika.
Serikali ya Kenya imebatilisha agizo lake la kuzifunga shule zilizoko eneo hilo la mau hadi mwezi ujao wanadunzi watakapokamilisha mitihani yao ya kitaifa.
Chanzo: DW Nakuru