Kenya: Mwanasheria mkuu amkosoa Raila kwa kutaka kujiapisha
7 Desemba 2017Hatua ya kiongozi wa upinzani nchini Kenya ya kujiapisha imepata pigo baada ya mwanasheria mkuu Githu Muigai kusema kuwa hatua hiyo ni uhaini na hukumu yake ni kifungo cha maisha. Akizungumza na wanahabari Muigai amesema hatua ya mabunge ya majimbo kupitisha miswada ya kuanzisha vikao vya mabunge ya wananchi pia ni kinyume cha sheria.
Aidha marekani imemtaka Odinga kutojiapisha ikisema ni ukiukwaji wa sheria. Wakati huo huo Odinga ameilani vikali jamii ya kimataifa kwa kunyamazia ukiukaji wa haki za binadamu baada ya uchaguzi mkuu uliotekelezwa na maafisa wa polisi.
Tamko la mwanasheria mkuu Githu Muigai linajiri siku nne kabla ya kiongozi wa upinzani raila Odinga kujiapisha kwa kutumia mabunge ya majimbo. Tayari majimbo 12 yamepitisha mswada wa kujenga vikao vya mabunge ya wananchi ambayo hayatambui uhalali wa rais Kenyatta. Kama ishara ambayo serikali ya rais Uhuru Kenyatta haitavumilia hatua ya Odinga, Muigai alisema.
Marekani yasema Raila Kujiapisha ni ukiukaji wa katiba
Kwenye hatua nyingine inaizima azma ya Odinga, ubalozi wa Marekani umeingilia kati suala hilo. Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari marekani imeitaja hatua hiyo kuwa inayokiuka katiba. Badala yake marekani imetaka upinzani kuzingatia njia za kisheria kutafuta mageuzi kwenye mchakato wa upigaji kura.
Taarifa hiyo inajiri wakati afisa mkuu wa marekani wa masuala ya Afrika Donald Yamamoto akiitembelea Kenya ambako kunashuhudiwa mgawanyiko wa kisiasa. Upinzani umesema kuapishwa kwa Odinga kumechangiwa na uchaguzi ambao rais Kenyatta alichaguliwa bila ya kuzingatia katiba na sheria. Odinga alisusia uchaguzi huo.
Upinzani wawafariji waliopoteza wapendwa wao
Wakati huo huo, kinara huyo wa upinzani alizuru hifadhi ya maiti ya City ambapo alijiunga ba familia za watu waliopoteza wapendwa wao baada ya uchaguzi. Upinzani ulizipa kila familia za waathiriwa shilingi elfu 50 mbali na kugharamia shughuli ya kusafirisha maiti kwa maziko.
Sasa Odinga anataka serikali iwape ridhaa waathiriwa. Tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu imeripoti kuwa watu 37 waliuawa na wengine 120 kujeruhiwa na maafisa wa polisi baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 26 mwezi Oktoba. Odinga ameongeza kuwa: "Wale wanafanya haya ni wanyama si binadamu, tunalaani vikali yale ambayo yamefanyika hapa. Tangu yafanyike hakuna hata mmoja kutoka kwa serikali ambaye amesema pole kwa wafiwa.”
Rais Uhuru Kenyatta aliapishwa baada ya kushinda uchaguzi uliofanyika tarehe 26 mwezi Oktoba na kuhalalishwa na mahakama ya Juu.
Raila ailaani jamii ya kimataifa kwa kunyamaza kimya
Odinga ameilani vikali jamii ya kimataifa kwa kuunyamazia ukiukaji wa haki za binadamu baada ya uchaguzi mkuu. Odinga ameeleza kuwa: "Tuna huzuni kwa vile hata mataifa wanaojiita marafiki wa Kenya hakuna hata mmoja wao amezungumza tangu yale yafanyike hadi leo kulaani upotevu wa maisha ya wakenya. Wakati ule mwingine kulikuwa na neno linaitwa haki, kulikuwa na mabolozi waliojitokeza na kuongea juu ya uvunjaji wa haki za bindamu katika taifa letu yale yote sasa hakuna.”
Kiongozi wa upinzani ametishia kujiapisha tarehe 12 mwezi huu huku akishikilia kuwa hamtambui Kenyatta kama rais aliyechaguliwa kwa njia halali.
Mwandishi: Shisia Wasilwa, DW, Nairobi