Kenya: Masomo yaanza tena Solai baada ya watoto 14 kufa
22 Mei 2018Shughuli za masomo zimeanza kurejea katika shule ya msingi ya Nyakinyua huko Solai, Nakuru, Kenya, mojawapo wa shule zilizoathiriwa pakubwa na kupasuka kwa bwawa la solai. Wanafunzi 14 kutoka shule hiyo walifariki katika tukio hilo, lililowaacha wengine bila makao, huku miundo mbinu ya shule ikiharibika. Ingawa mmoja baada ya mwingine wanawasili kuendeleza masomo yao, kumekuwa na hali ya simanzi na mshtuko miongoni mwa waalimu na wanafunzi.
Wanafunzi hawa katika shule ya msingi ya Nyakinyua, kaunti ya Nakuru wanaonekana wenye wasiwasi. Wamejikunyata kwenye vikundi, polepole wakijadili matukio ya takriban majuma mawili yaliopita. Wengi waliwapoteza wapendwa wao katika mkasa ambapo bwawa la Solai lilivunja kingo zake na kusababisha mafuriko katika vijiji jirani. Kati ya watu 47 waliofariki 14 walikuwa wanafunzi wenzao, ambao hii leo nafasi zao darasani zimesalia wazi. Lakini, azma yao kuu wanapowasili hapa ni kwa ajili ya kupata msaada utakaowawezesha kuendelea na masomo yao.
Marehemu walizikwa katika kaburi la pamoja
Wanafunzi wa shule hiyo waliofariki walizikwa katika kaburi la pamoja umbali wa mita 200 kutoka madarasa ya shule hiyo. Usimamizi wa shule unaposubiri msaada kutoka kwa serikali, mikakati imewekwa kuwatafuta washauri nasaha na viongozi wa kanisa, kufika hapo ili kuwaliwaza na kuwaondolea kiwewe wanafunzi kufuatia waliyoyashuhudia.
Kinyanjui Kihanya ambaye ni naibu mkuu wa shule hiyo, anasema baadhi ya wanafunzi hao waliripoti mapema shuleni, ingawa wengi wao hawana sare za shule na vitabu. Aidha baadhi ya madarasa yaliharibiwa huku mengine yakikosa madawati na vifaa vingine muhimu.
Miundo mbinu muhimu yakosekana
Waalimu na wanafunzi wamesalia kutumia vyoo vya muda vilivyotengezwa kuwahudumia, lakini ni muda tu kabla idadi hiyo ya wanafunzi 500 iwe kubwa zaidi kuimudu na kusababisha athari zingine.
Shule jirani ya upili ya Solai iliokuwa mwenyeji wa familia zilizoathirika na mafuriko wakati wa tukio la Solai pia imefunguliwa. Manusura waliokuwa wakiishi hapo kwa takriban wiki mbili waliondolewa baada ya kupewa msaada na serikali kuwawezesha kuanza upya maisha yao.
Mwandishi: Wakio Mbogho, DW Nakuru.
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman