1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kuwapa wafanyakazi wa umma wa DRC mafunzo

Thelma Mwadzaya7 Februari 2019

Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimeahidi kufungua uhusiano mpya ambao utaiwezesha Kenya kuwapa wafanyakazi wa umma wa DRC mafunzo.

https://p.dw.com/p/3Ctlt
Kenia Uhuru Kenyatta und Felix Tshisekedi
Picha: PSCU

Kenya imefungua ukurasa mpya wa uhusiano na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo baada ya kuahidi kuwapa mafunzo wafanyakazi wake wa umma katika harakati za kuiunga mkono serikali mpya ya Rais Felix Tshisekedi. Tshisekedi anayazuru mataifa ya Afrika, wiki mbili tangu alipoapishwa kuiongoza nchi hiyo, ambapo Uhuru Kenyatta ndiye rais pekee aliyehudhuria hafla ya kumuapisha Tshisekedi.

Kwenye kikao cha alasiri siku ya Jumatano, akiwa kwenye Ikulu ya Nairobi Rais Uhuru Kenyatta alimuahidi mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Felix Tshisekedi kuwa atawaunga mkono ili kuleta ustawi wa kisiasa katika nchi hiyo iliyotatizwa na vurugu wakati wa uchaguzi mkuu wa Disemba iliyopita.

Ili kufanikisha ahadi hiyo, wafanyakazi wa umma wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo watapewa mafunzo ya uongozi katika baadhi ya vyuo hapa nchini kama vile Kenya kama vile Chuo cha Mafunzo ya kiserikali cha Kenya (Kenya School of Government). Dhamira ni kutimiza ndoto za waasisi wa mataifa ya afrika kwa manufaa ya ujirani mwema aliweka bayana Rais Uhuru Kenyatta.

Kuhusu masuala ya biashara, viongozi wa mataifa hayo mawili wameahidi kuimarisha ushirikiano ukizingatia kuwa bidhaa nyingi za Congo zinapitia bandari ya Mombasa zikielekea miji ya Goma na Lubumbashi iliyoko mashariki mwa Jamhuri hiyo.

Rais Tshisekedi aliyeapishwa Januari 24, anafanya ziara yake ya kwanza ya kigeni katika baadhi ya nchi za Afrika.
Rais Tshisekedi aliyeapishwa Januari 24, anafanya ziara yake ya kwanza ya kigeni katika baadhi ya nchi za Afrika.Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Kwa upande wake, Rais Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo alimshukuru mwenyeji wake kwa kuwa rafiki wa dhati wa taifa lake hasa baada ya kuhudhuria hafla ya kumuapisha rasmi siku chache zilizopita. Rais Tshisekedi kadhalika alikiri kuwa bandari ya Mombasa ina mchango na umuhimu mkubwa na kuwa wako tayari kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuimarisha biashara ya kikanda.Viongozi hao wawili wameahidi kutembeleana pindi Rais Tshisekedi atakapounda serikali yake mpya.

Kwa upande mwengine Rais Tshisekedi alikutana pia na mjumbe maalum wa umoja wa Afrika, Raila Odinga kwenye afisi yake ya Capitol Hill siku ya Jumatano.Raila alimrai kuwa thabiti kuepusha mpasuko utakaowapa mwanya wasioitakia mema Congo kutokea nchi za kigeni na kumpongeza kwa kurithi madaraka kwa amani.

Rais Tshisekedi alianzia ziara yake ya kwanza tangu kuapishwa nchini Angola siku mbili zilizopita, na itamalizikia katika Jamhuri ya Congo jijini Brazzaville.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya

Mhariri: Iddi Ssessanga