Kenya kutobadili timu ya Marathon Olimpiki Tokyo
25 Februari 2021Timu hiyo inayoongozwa na bingwa mtetezi wa Marathon ya Olimpiki Eliud Kipchoge, na anayeshikilia rekodi ya dunia kwa upande wa wanawake Brigid Kosgei, inatarajiwa kuripoti kambi ya mazowezi mjini Kaptagat, kaskazini-magharibi mwa Kenya Machi 3.
"Tunabakisha timu ile ile iliyochaguliwa kwa ajili ya marathon kabla ya kuahirishwa kwa michezo ya Olimpiki ya Tokyo kutokana na janga la covid-19," alisema mjumbe mtendaji wa Kamati ya Riadha Kenya (AK), Bernabas Korir katika mazungumzo na shirika la habari la AFP.
"Wanariadha waliochaguliwa wako katika ubora wao wa hali ya juu kabisaa tayari kushindana baada ya mwaka mzima wa kutokuwa na cha kufanya kutokana na janga. Hakuna haja ya kubadili timu ya ushindi."
Timu ya wanaume inajumuisha bingwa wa sasa wa mashindano ya Boston na Chicago Lawrence Cherono na mshindi wa medali ya shaba wa mashindano ya ubingwa wa dunia yaliyofanyika Doha, Amos Kipruto.
Kosgei ambaye aliweka rekodi ya dunia ya wanawake ya masaa 2:14.4 katika Marathon ya Chicago, atashindana na bingwa wa sasa wa Marathon ya dunia Ruth Chepngetich, na mshindi wa zamani wa dhahabu katika mbio za mita 5,000 na 10,000 Vivian Cheruiyot.
Timu hiyo ya marathon inaungana na wanariadha wengine wanaoanza mazoezi wiki ijayo katika kambi maalumu, kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa wa covid-19.
Kenya, ambayo ni taifa kubwa katika riadha duniani, ilimaliza katika nafasi ya 15 na ikiwa ya kwanza Afrika katika mashindano ya riadha ya mwaka 2016 mjini Rio de Janeiro, ikiwa na jumla ya medali 13 - sita za dhahabu, sita za fedha na moja ya shaba.
Kenya pia iliongoza kwenye jedwali jumla la medali kwenye mashindano ya riadha ya ubingwa duniani ya mwaka 2015 mjini Beijing, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia yake, baada ya kushinda medali saba za dhahabu, sita za fedha na tatu za shaba.