Kenya kuahirisha muda wa kufunga Dadaab
15 Novemba 2016"Kuhusiana na swala la muda huo wa mwisho, ni wazi kwamba hatutaafikia malengo yaliowekwa," Mwenda Njoka msemaji wa wizara hiyo ya usalama wa kitaifa aliliambia shirika la habari la Reuters katika tangazo la kwanza la hadharani kuhusiana na kushindwa kwa Kenya kuifunga kambi ya Dadaab kwa muda iliokuwa imeuweka.
Wataalamu walikuwa wamesema kuwa uamuzi huo wa Kenya wakutaka kufunga kambi hiyo ya Dadaab ambayo ni makazi ya wakimbizi wengi miaka michache iliyopita kufikia tarehe hiyo lilikuwa jambo gumu kutekelezeka.
Njoka alisema kuwa kambi hiyo kubwa zaidi duniani kwa sasa ilikuwa na takriban wakimbizi elfu 250. Idadi hiyo inalinganishwa na takriban watu elfu 350 ambao maafisa wa umoja wa mataifa wanasema waliishi katika kambi hiyo iliyoko Kaskazini Mashariki mwa Kenya mwanzoni mwa mwaka huu .
Wataalamu wanasema kuwa raia wengi wa Somalia waliokimbia ghasia nchini mwao hawawezi kurejea nchini humo kwa hiari hadi pale usalama utakapoimarishwa pamoja na huduma nyingine muhimu kama vile shule na vituo vya afya vitakapowekwa. Serikali ya Somalia bado inakabiliana na tatizo la ugaidi.
Njoka aliendelea kusema kuwa wataendelea kushirikiana na serikali ya Somalia pamoja na jimbo la somalia linalojitawala la Jubbaland kwa lengo la kutafuta njia ya kukamilisha hatua hiyo kwa haraka .
Jimbo la Jubbaland liko karibu na mpaka wa Kenya.
Mwingilio wa nje kushinikiza kutofungwa kwa kambi hiyo
Kenya ilikuwa imesema kuwa imeamua kufunga kambi hiyo ambapo baadhi ya wakimbizi wenye umri mkubwa wameishi katika eneo hilo kwa miaka mingi na baadhi ya vijana wameishi katika eneo hilo maisha yao yote, kwa sababu ya kitisho kwa usalama wake. Kenya pia imekabiliwa na misururu ya mashambulizi kutoka kwa wanamgambo wa kiislamu.
Umoja wa mataifa na mataifa ya Magharibi zilikuwa zimeionya Kenya kutowarejesha wakimbizi hao nchini mwao kwa lazima kutoka kwa kambi hiyo inayosimamiwa na umoja wa mataifa . Kundi moja la kufuatilia haki la kibinadamu lenye makao yake mjini Newyork, mnamo mwezi Septemba lilisema kuwa baadhi ya maafisa wanawashinikiza wakimbizi hao kuondoka .
"inatuuma sana wakati watu wanasema tunawashinikiza watu hawa kuondoka," alisema Njoka, na kuongeza kuwa kati ya mwezi Mei na Oktoba, zaidi ya watu elfu 30 walikuwa wameondoka kwa hiari.
Njoka aliendelea kusema, " iwapo tulikuwa tunawalazimisha kuondoka, kwa nini bado tuko na watu elfu 250 katika kambi hiyo? hamuoni kwamba tungekuwa tumewafurusha wote?
Shirika la umoja wa mataifa linaloshugulikia wakimbizi UNHCR pamoja na Somali zilitia saini mkataba wa kuondoka kwa wakimbizi kwa hiari mnamo mwaka 2013, uliolenga kufunga kambi hiyo. Mkataba huo unafika kikomo mwisho wa mwezi huu na Njoka amesema kuwa itabidi mkataba huo kujadiliwa upya .
Huku maeneo mengi ya Somalia yakiwa salama kwa wakimbizi hao kurejea , hawana miundo msingi hasa katika maeneo kama vile jimbo la Jubbaland, alisema Njoka na kuongeza," kwa hivyo hali hiyo imetatiza utekelezaji wa hatua hiyo".
Mwandishi: Tatu Karema/ RTRE
Mhariri: Gakuba Daniel