Kenya yakabiliwa na duru mpya ya maandamano
19 Julai 2023Maeneo kadhaa ya nchi yakiwemo mitaa mbalimbali ya Nairobi na Kisumu kwa sasa yanashudia makabiliano kati ya waandamanaji na polisi. Polisi wanawafyatulia mabomu ya kutoa machozi waandamanaji wanaoonekana kuwasha moto matairi barabarani.
Upinzani umeapa kufanya maandamano kwa siku tatu mfululizo
Upinzani umeapa kufanya maandamano kwa siku tatu mfululizo dhidi ya serikali ya Rais William Ruto, na kusababisha jumuiya ya kimataifa kujiunga katika kutoa wito wa kupatikana suluhisho la kisiasa katika mzozo huo. Shule za kutwa na maduka yamefungwa katika mji mkuu wa Nairobi na miji mingine, huku waandamanaji wakihimizwa kubeba sufuria na kuingia mitaani.
Hii ni mara ya tatu Raila Odinga aandaa maandamano makubwa
Hii ni mara ya tatu ndani ya mwezi huu kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuandaa maandamano makubwa dhidi ya serikali anayosema si halali na inahusika na mgogoro wa kupanda gharama ya maisha.