Miaka 20 tangu kunyongwa Ken Saro-Wiwa
10 Novemba 2015Tukio hilo la kunyongwa Ken Saro-Wiwa lilishituwa Ulimwengu mzima, baada ya serikali ya Kijeshi nchini humo kupuuza wito wa kimataifa, kuwanusuru wanaharakati hao .
"Ogoni iliokubwa, ardhi ya heshima, Ogoni kubwa, ardhi yenye utajiri. Ninawaonya watu wa Ogoni, hatutapambana kwa mapanga, mapambano yetu ni ya hekima na amani. Hapapaswi kumwagwa damu, ” alisema Ogoni Ken Saro-Wiwa, mpigani haki za watu wa Ogoni.
Ken Saro-Wiwa aliyekuwa mwandishi vitabu na mwanaharakati aliyepigania haki ya watu wa Ogoni nchini Nigeria kutaka wafaidike na utajiri wa mafuta wa ardhi yao, alinyongwa mjini Port harcourt 1995 baada ya kuhukumiwa kifo na mahakama ya kijeshi. Hayo yalifuatia uasi uliofanyika kwa njia ya amani wa wakaazi wapatao 300,000 wa eneo hilo dhidi ya kampuni ya mafuta ya kimataifa ya Shell Januari 4 mwaka 1993.
Malalamiko ya jumuiya za kimataifa
Kunyongwa kwa Saro Wiwa kulisababisha malalamiko makali kutoka jamii ya kimataifa na Nigeria ikasimamishwa uwanachama wake katika Jumuiya ya madola ya Commonwealth, inayozileta pamoja Uingereza na makoloni yake ya zamani katika sehemu mbali mbali duniani.
Kilio cha watu wa Ogoni kilikuwa na bado kinaendelea kuwa kupigania haki ya utajiri wao,kutokana na kufaidika kwa kampuni ya Shell na serikali ya Nigeria huku eneo hilo likiachwa kuwa masikini bila ya maendeleo ya aina yoyote. Mbali na kuyapigania hayo Ken Saro-Wiwa aliongoza kampeni kubwa dhidi ya uharibifu wa mazingira unaosababishwa na kampuni la Shell na makampuni mengine ya mafuta.
“Dunia imeona jinsi watu wa Ogoni walivyozindukana. Wameona kwamba serikali inawahadaa na Shell inatuangamiza,” alisema Ken saro-Wiwa kabla ya kuhukumiwa kifo.Miaka 30 hadi eneo kusafika
Mwanawe Saro-Wiwa anayeitwa pia Ken, na ambaye aliteuliwa na Rais wa zamani wa Nigeria kuwa mshauri wake, anasema hivi sasa Ogoni iko kwenye ramani ya dunia na kwamba makampuni ya mafuta yanabeba dhamana ya kushindwa kulisafisha eneo hilo kutokana na miongo kadhaa ya uharibifu wa mazingira. Anasisitiza kwamba mabadiliko ya tabia nchi ni suala kuu katika kipindi cha nusu ya karne ya 21 na kadhia ya Ogoni ni sehemu ya suala hilo .
Licha ya kampuni ya Shell , serikali ya Nigeria na wadau wengine kukubali kutekeleza ripoti ya Umoja wa mataifa kusawazisha athari za mazingira katika eneo hilo la Ogoni, bado kasi ni ndogo.
Umoja wa Mataifa unaashiria itachukuwa alau miaka 30 kulisafisha eneo hilo kutokana na uharibifu wa mazingira wa makampuni ya mafuta.
Mtoto Ken anasema bado watu wananjaa na shauku kuhusiana na suala hilo na ukosaefu wa imani ni mkubwa. Pamoja na kwamba ulimwengu umezindukana kufuatia juhudi za Ken Saro-Wiwa na kulitambua janga la watu wa Ogoni lakini ni faraja ndogo tu, kwa sababu maafa bado yanaendelea.
Mnamo wiki iliopita, kampuni ya Shell ilishutumiwa kwamba inatoa madai yasio ya kweli kuhusu kiwango cha kusafisha uharibifu wa shughuli zake nchini Nigeria na kuitaka ichukuwe hatua zaidi kuisaidia jamii ya eneo hilo. Katika kuikumbuka siku ya kunyongwa mwanaharakati Ken-Saro Wira na wenzake wanane ukiwa ni mwaka wa 20, wanaharakati wamepanga kuandamana nje ya vituo vya mafuta vya Shell , ili kulishinikiza liwajibike.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman /: Morgenrath,Birgit
Mhariri:Yusuf Saumu