1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kazi tuliyotumwa Iraq tumeimaliza-Jeshi la Uturuki.

Kalyango Siraj29 Februari 2008

Lakini kweli kazi imemalizika?

https://p.dw.com/p/DFrz
Msururu wa malori ya kijeshi ya Uturuki yakiwa yamejaa askari yakirudi kutoka kaskazini mwa Iraq Ijumaa, Feb. 29, 2008. Jeshi linasema limemaliza kazi lililotumwa kuwasaka waasi wa PKK Iraq.Picha: AP

Vikosi vya Uturuki vimekamilisha operesheni yake dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi kaskazini mwa Iraq.Vikosi hivyo sasa vimeanza kurejea nyuma.

Hata hivyo haijulikani hatua hiyo imetokana na kufanikiwa katika lengo lake ama kwa ajili ya shinikizo la kimataifa.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uturuki-Hoshyar Zebari,amesema Ijumaa kuwa majeshi ya Uturuki yamemaliza operesheni ya wiki nzima kaskazini mwa Iraq iliowahusisha wanajeshi karibu elf 10.

Lengo lake lilikuwa kuharibu maficho ya wapiganaji wa kikurdi wa Kurdistan Worker's Party- maarufu kama PKK.Wapiganaji hao wamekuwa wakishambulia vituo vya kijeshi na wakati mwingine raia wa kawaida ndani ya Uturuki.

Serikali ya Ankara inadai kuwa wapiganaji hao wamekuwa wakitumia maficho yao ndani ya Iraq na miito kadhaa kwa serikali ya Baghdad kuwazuia hazikuzaa matunda.Ndio ikaibidi kuchukua hatua kama hiyo.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki amesema kuwa majeshi yameanza kuondoka.

Msemaji wa PKK amenukuliwa na vyombo vya habari vya nchi za magharibi akisema kuwa majeshi ya Uturuki yamerejea nyuma kutoka katika eneo la Zap-ambalo kunapatikana ngome kuu ya wapiganaji hao ambayo iko karibu na mpaka wa Iraq na Uturuki.

Kituo kimoja cha Televisheni nchini Uturuki kimeonyesha picha ambazo zinaonyesha magari ya kijeshi yaliyojaa wanajeshi yakivuka mpaka yakiingia Uturuki huku mengine matupu yakivuka yakielekea upande wa Iraq.

Haieleweki ikiwa majeshi yote yaliyoanza kuingia kaskazini mwa Iraq Febuari 21 yote yameondolewa.Afisa mmoja wa kijeshi amekiambia kituo kimoja cha Televisheni nchini Uturuki kuwa ni vile vikosi tu ambavyo vimekamisha zamu yake ndio vinarejea nyumbani.Hili likiashiria kuwa vikosi vingine vinaweza kubaki ndani ya Iraq.

Viongozi wa kisiasa pamoja na wa kijeshi wa Uturuki, akiwemo waziri wa Ulinzi wa Uturuki-Vecdi Gonul walisikika wakisema kuwa operesheni itaendelea hadi pale kazi yote imekamilika.

Lakini wamekabiliwa na shinikizo kutoka Marekani na washirika wao katika umoja wa kujihami ya Ulaya wa NATO kufupisha operesheni yao hii na pia kulenga tu shabaha yao.

Alhamisi rais George W Bush wa Marekani aliihimiza Uturuki kusitisha operesheni ya majeshi yake ya nchi kavu nchini Iraq.

Marekani, Umoja wa Ulaya na Ankara zinalichukulia kundi la PKK kama kundi la kigaidi na zimekuwa zikilipa jeshi la Uturuki habari za kijasusi kuwahusu wapiganaji wa PKK nchini Iraq.Lakini utawala wa Washington unaogopa kuwa kuendelea kwa operesheni hiyo ya Uturuki kunaweza kukaleta hali ya wasiwasi katika eneo hilo.

Jeshi la Uturuki linasema kuwa limewauwa wapiganaji 237 na kupoteza wanajeshi 24 katika operesheni iliochukua siku nane.

Wao wapiganaji wa PKK wanadai kuwa wamewauwa wanajeshi zaidi ya 100,lakini hawakutoa hasara walioipata.

Uturuki inadai kuwa watu wanaofikia elf 40 wameuawa na wapiganaji hao tangu mwaka wa 1984.

Operesheni hii ndio ya kwanza kwa uturuki ndani mwa Iraq ikitumia wanajeshi wengi wa nchi kavu.Duru za kuaminika zinasema wametumiwa takriban wanajeshi wa nchi kavu wapatao elf 10.