1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu Mkuu wa UN alaani uvamizi uliofanywa Somalia

Kabogo Grace Patricia22 Julai 2009

Hata hivyo, Ban Ki-Moon amesema UN itaendelea na shughuli zake za kutoa misaada.

https://p.dw.com/p/Iv5g
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon.Picha: AP

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amelaani uvamizi uliofanywa katika afisi za Umoja wa Mataifa nchini Somalia, lakini akasisitiza Umoja huo utaendelea na shughuli zake za kutoa misaada katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inayokabiliwa na misukosuko na vita vya mwongo mzima sasa. Umoja wa Mataifa ulisimamisha kwa muda shughuli zake katika mji wa Baidoa baada ya wavamizi kuharibu mitambo na kuiba vifaa katika afisi ya Umoja huo.

Shutma hizi kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, zinafuatia uvamizi uliotekelezwa na wanamgambo wa Kiislamu katika afisi ya Umoja huo-katika mji wa Baidoa. Lengo lake ilikuwa kulemaza shughuli za usambazaji wa misaada zinazofanywa na Umoja wa Mataifa nchini Somalia.

Kulingana na maafisa wa Umoja wa Mataifa- watu waliokuwa na bunduki walivamia eneo lenye majengo ya afisi za UNDP, shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa na afisi ya kisiasa ya Umoja huo, baada ya wapiganaji wa kiislamu kusitisha shughuli zinazoendeshwa na Umoja huo kwa kisingizo kwamba Umoja wa Mataifa ulikuwa ni adui ya Waislamu.

Wavamizi hao walifanikiwa kutoroka na vifaa na mitambo ya mawasiliano ya dharura vilivyokuwa katika afisi hizo. Vifaa vingine kama Kompyuta, tarakilishi na stakabadhi zingine za afisi ziliharibiwa.

Msimamizi wa shughuli za kutoa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, John Holmes, alisema wamesimamisha kwa muda shughuli zao katika mji wa Baidoa, lakini akasisitiza wataendelea na operesheni zao watakapopata vifaa vingine.

Holmes lakini alikuwa mwepesi kuunga mkono matamshi ya Ban Ki-moon kwamba Umoja wa Mataifa hautovunjika moyo na kusimamisha miradi yake nchini Somalia kufuatia mashambulio hayo. Somalia ndio eneo la nne kubwa duniani ambalo Umoja wa Mataifa husambaza misaada ya kibinadamu.

Wakati huo huo, shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, limetangaza kwamba katika wiki mbili zilizopita zaidi ya watu 20,000 wametoroka makaazi yao katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, kufuatia kuchacha kwa vita kati ya wanamgambo wa Kiislamu na wanajeshi wa serikali.

Jumla ya wakimbizi zaidi ya laki mbili hawana makao nchini Somalia tangu mwezi Mei, pale wapiganaji wa Kiislamu Al-Shabab walipoanzisha vita vya kujaribu kuipindua serikali ya Rais Sheikh Sharrif.

Shirika la UNHCR linasema lina wasiwasi kufurika huku kwa wakimbizi wa ndani kwa ndani nchini Somalia, kunazidi kuzorotesha hali ya wakimbizi nchini Somalia kwa kukosekana mahitaji ya kimsingi, kama maji safi, vyakula, madawa na makaazi.

Na hatimaye hali ya raia wawili wa Ufaransa waliotekwa nyara nchini Somalia wiki moja iliyopita inazidi kuzongwa na utata. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Bernard Kouchner, alinukuliwa akisema maafisa hao wawili wametenganishwa na kwamba wanazuiliwa na makundi mawili tofauti .

Kouchner aliongeza kusema Ufaransa imeanzisha mazungumzo na watekaji nyara hao kuhusu kuachiliwa huru kwa raia hao wawili, kupitia ubalozi wa Ufaransa mjini Nairobi. Maafisa hao wawili waliokuwa nchini Somalia kutoa mafunzo kwa jeshi la Serikali walitekwa nyara katika hoteli waliyokuwa wanaishi mji ni Mogadishu wiki moja iliyopita.

Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE

Mhariri: Miraji Othman