Guterres na wajumbe wa kimataifa kuijadili Afghanistan
30 Aprili 2023Katibu Mkuu wa Umioja wa Mataifa Antonio Guterres, anatarajiwa hapo kesho Jumatatu kukutana na wajumbe wa kimataifa mjini Doha, katika juhudi za kutafuta njia za kuwashawishi watawala wa Afghanistan. Umoja wa Mataifa umezidi kuingia katika kuzungumkuti baada ya utawala wa Taliban kuamua kuwakataza wasichana kwenda shule na kuwazuia wanawake kufanya kazi hata kwenye mashirika ya Umoja wa Mataifa. Hata hivyo wataliban walioingia madarakani tangu mwaka 2021 hawatawakilishwa kwenye mkutano huo wa mjini Doha. Wajumbe kutoka nchi zipatazo 25 watahudhuria mkutano huo pamoja na mashirika ya kimataifa. Wakati huo huo Umoja wa Mataifa na mataifa ya magharibi yamehakikisha kwamba suala la kutambuliwa serikali ya Wataliban halitajadiliwa kwenye mkutano huo. Guterres atatoa muhtasari juu ya shughuli za misaada muhimu inayotolewa na Umoja wa Mataifa kwa watu wa Afghanistan.