Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ahimiza kukubali mkataba mpya wa hali ya hewa
12 Desemba 2007Katibu Mkuu wa Umoja waMatifa-Ban Ki Moon ameuhimiza ulimwengu kukubali kutayarisha mkataba mpya kuhusu hali ya hewa ifikapo mwaka wa 2009 na kuongeza kuwa maelezo zaidi kuhusu mkataba huo yatashughulikiwa baabda ya mazungumzo ya Bali.
Kinara wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito huo wakati akihutubia mkutano wa mawaziri wa mazingira zaidi ya 120 walioko Bali kujadilia jinsi ya kupata mkataba mpya wa hali ya hewa utakao chukua ule wa Kyoto ambao utamalizika hivi karibuni.
‚…ikiwa tutaondoka bali bila ya mafanikio yoyote,tutakuwa sio tu tumewapuuza viongozi wetu viongozi wetu lakini pia na wale wanaotutegemea kupata ufumbuzi ambao ni watu wa dunia hii…’ amesema Ban Ki -moon
Akigusia mvutano kati ya Marekani na umoja wa Ulaya na baadhi ya nchi zinazoendelea, Ban Ki Moon, amesema lengo la mkutano wa Bali ni kukubali kuzindua mdahalo kuhusu mkataba utakao chukua pahala pa ule wa Kyoto. Ameuambia mkuatano huo kuwa kubadilka kwa hali ya hewa ni moja wa changamoto kubwa ya kizazi hiki na kuongeza kuwa kuna haja ya kuchapuza juhudi ili kukabiliana dhidi ya kupanda kwa kima cha maji ya bahari, mafuriko, ukame, njaa na kutoweka kwa wanyama.
Marekani ndio iko mstari wa mbele kupinga kile kinachoelezewa kama ushahidi wa kisayansi kuwa kuna haja ya kupunguza gesi chafu.Kiwango kinachopendekezwa ni kati ya asili mia 25 na 40 ifikapo mwaka wa 2020, hii kikiwa kiwango cha chini sana kutoka kile cha mwaka wa 1990.Hii imependekezwa kama mwongozo.
Yeye rais wa Indonesia- Susilo Bambang Yudhoyono ametoa mwito wa kufanyika juhudi za kuihusisha Marekani katika hatua za sasa.
‚…lazima tuhakikishe kuwa Marekani kama taifa tajiri duniani,na mabalo sio tu ni namba moja kwa utoaji wa gesi chafu lakini pia kuongoza katika teknolojia inakuwa sehemu ya mpango huu…,’amesema Bambang
Nayo serikali ya Austaralia kwa upande wake imeahidi kufanya kila iwezalo kuona kuwa inatekeleza mapendekezo ya hali ya hewa.Waziri mkuu wake, Kevin Rudd,baada ya kuwasilisha hati maalum za kuukubali mkataba wa Kyoto,ameuambia mkutano huo kuwa nchi yake iko tayari.
‚…Serikali ya Australia imepania kupunguza gesi zake inazotoa kwa asili mia 60 ifikapo mwaka wa 2012. Australia itatekeleza mpango wa mafunzo kuhusu utoaji wa gesi chafu ifikapo mwaka wa 2010,ili kufikia shabaha yake.Ifikapo mwaka wa 2020 tutakuwa tumeongeza uwezo wetu wa nishati endelevu kwa asili mia 20’,asema Rudd.
Umoja wa Ulaya umesisitiza kuwa nchi tajiri zinahijakila kuonyesha mfano mzuri wa kuweza kuzishawishi zile zinazoendelea kama vile China na India kuanza kupunguza gesi zao ambazo zinaongezeka kila kukicha.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameziomba nchi zote duniani,ikiwemo Marekani kutokuwa na msimamo mkali kueleka suala hilo.
‚…sote kwa pamoja tunawajibika na tatizo hili la ujoto duniani. Kwa hivyo sote kwa pamoja tushirikiane kupata ufumbuzi. Na mwanzo ni hapa bali.Ebu tubadilishe hali ya hewa kuwa mgogoro bali iwe uzima’ amesema Ban Ki -moon.
Mawaziri wa mazingira watajadiliana hadi Ijumaa.