1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu Mkuu wa NATO atarajiwa Uturuki.

Abdu Said Mtullya27 Agosti 2009

Rasmussen ataka mchango mkubwa zaidi kutoka Uturuki.

https://p.dw.com/p/JJJ2
Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen akizungumza na mwanajeshi.Picha: AP

Katibu Mkuu wa jumuiya ya kijeshi ya Nato Anders Fogh Rasmussen ameitaka Uturuki itoe mchango mkubwa zaidi katika harakati ya kupambana na ugaidi nchini Afghanistan.

Bwana Rasmussen ametoa mwito huo mjini Athens ambako amefanya mazungumzo juu ya mgogoro wa Ugiriki na Uturuki.

Katibu mkuu wa Nato anaetarajiwa kuwasili nchini Uturuki leo , amesema ni juu ya nchi za Nato kuamua namna ya kutoa michango yao katika harakati za nchini Afghanistan.Lakini amesisitiza kuwa litakuwa jambo muhimu ikiwa nchi wanachama zitapeleka majeshi.

Katibu mkuu huyo amesema lengo la muda mrefu la Nato nchini Afghanistan ni kuwawezesha watu wa nchi hiyo kuwajibika juu ya usalama wao.

Katibu Mkuu wa Nato bwana Rasmussen amesema jumuiya hiyo inaunga mkono hatua za kupeleka majeshi nchini Afghanistan.

Uturuki mpaka sasa ina askari wa nchi kavu 730 katika jeshi la kimataifa linaloongozwa na Nato nchini Afghanistan.

Lakini jukumu la askari hao wa Uturuki linaishia katika mji mkuu ,Kabul na katika sehemu zilizopo karibu na mji huo.

Uturuki ambayo ni mwanachama mwislamu wa Nato imeashiria utayarifu wa kuongeza idadi ya askari wake nchini Afghanistan.

Katibu mkuu wa Nato amesema anaamini, kuwepo kwa wanajeshi wa kiislamu katika mapambanano dhidi ya taliban na alkaida nchini Afghanistan kutasaidia kuzielewesha nchi nyingine za kiislamu kwamba harakati za Nato nchini Afghanistan siyo vita vya kidini bali ni harakati za kupambana na ugaidi.

Uturuki ilisimama kidete kumpinga Rasmussen aliekuwa waziri mkuu wa Denmark, wakati aliposimama kugombea ukatibu mkuu wa Nato.Uturuki ilimpinga kwa sababu alitetea kuchapishwa, kwenye magazeti ya Denmark, kwa vibonzo vilivyomkashifu mtume wa dini ya kiislamu Mohammad.Mkasa huo ulisababisha zogo kubwa miongoni mwa nchi za kiislamu mnamo mwaka 2005.

Katibu mkuu Rasmussen leo jioni atafuturu na waziri mkuu wa Uturuki Bwana Erdogan.

Bwana Rasmussen anafanya ziara katika miji mikuu ya nchi za Nato kwa lengo la kuleta uhusiano wa ndani miongoni mwa wanachama wa jumuiya hiyo.

Wakati huo huo Ugiriki imesema ipo tayari kushirikiana na Uturuki katika mfungamano wa Nato.

Hapo awali katibu mkuu wa Nato alikuwapo mjini Athens katika juhudi za kusuluhisha katika mgogoro wa Uturuki na Ugiriki.

Mwandishi/ Mtullya Abdu/AFPE

Mhariri/M.Abdul-Rahman.

.