1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu mkuu wa Nato ataka muungano huo kuwa kitu kimoja

17 Februari 2017

Katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg, amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa ulinzi wa hali ya juu baina ya mataifa ya Ulaya na Marekani.

https://p.dw.com/p/2XmTf
Belgien Jens Stoltenberg NATO PK
Katibu mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: Reuters/F. Lenoir

Alipokuwa akiwasili kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa usalama uliofunguliwa Munich, Ujerumani siku ya Ijumaa, Stoltenberg alisema kwamba hiki ni kipindi ambacho kuna misukosuko mingi na hali ya kutoeleweka na kutokana na hilo kunastahili kuwepo muungano utakaoyaweka mataifa pamoja. Katibu huyo mkuu wa NATO alieleza kwamba mkutano wa mawaziri wa ulinzi uliokamilika jana huko Brussels, Ubelgiji ulitoa ujumbe wa wazi kwamba Ulaya na Marekani wote wanaunga mkono kuungana kwao ili kukabiliana na changamoto zilizoko.

Aliusisitiza ujumbe wa waziri wa ulinzi wa Marekani James Mattis kwamba anatarajia mataifa wanachama wa NATO watekeleze yale waliyokubaliana, yakiwemo kuongeza bajeti ya masuala ya ulinzi ambapo lengo waliloweka ni la kufikia angalau asilimia mbili ya bajeti nzima katika kipindi cha mwongo mmoja, jambo alilokiri kwamba litahitaji muda zaidi kwa baadhi ya mataifa.

NATO inataka mazungumzo na Urusi

"Baada ya miaka ya kupunguza matumizi, mataifa wanachama wa NATO wamekubaliana kuongeza matumizi. Na jana tu, Romania ilitangaza kwamba itakifikia kile kiwango cha asilimia mbili mwaka huu, jambo linaloongeza nchi moja zaidi kwenye ile idadi ya nchi zinazotumia asilimia mbili au zaidi kwenye ulinzi," alisema Stoltenberg alipokuwa akiwahutubia waandishi wa habari.

Katibu huyo mkuu wa NATO pia alisema kwamba kuna umuhimu wa kufanya mazungumzo na Urusi, hasa wakati huu ambapo harakati za kijeshi zinaendelea katika maeneo ya mpakani huku kukiwa na taharuki ya kiwango cha juu.

Schweden Donald Tusk in Stockholm
Rais wa baraza la Ulaya Donald Tusk atarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa Munich piaPicha: Getty Images/AFP/M. Ericsson

"NATO ina msimamo wa wazi kwamba inataka mazungumzo na Urusi, tunatazamia kuwa na uhusiano mzuri mno na Urusi. Urusi ni jirani wetu mkubwa hasa wakati huu ambapo harakati za kijeshi zinafanywa mipakani, ninaamini kwamba kuna haja kubwa ya mazungumzo baina ya NATO na Urusi," alisema katibu huyo mkuu wa NATO.

Viongozi akiwemo Kansela Angela Merkel kuhudhuria mkutano huo

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk ni miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa kushiriki mkutano huo ambao unatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi zaidi ya 30 pamoja na mawaziri 80 wa wizara ya mambo ya nje na ulinzi pamoja na maafisa kadhaa.

Mkutano huo unafanyika wakati Rais Trump akiwa tayari ametoa kauli kadhaa kuhusiana na Jumuiya hiyo ya kujihami na hivi karibuni  akitoa kauli inayooonyesha kukubaliana na umuhimu wa ushirikiano huo wa kijeshi. Hata hivyo, amesisitiza juu ya  haja ya kila nchi mwanachama  wa ushirikiano huo kutoa mchango wake kikamilifu kuhusiana na masuala ya ulinzi jambo ambalo viongozi wa NATO wamekuwa wakilipigania kwa muda mrefu.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba