Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO ziarani mjini Moscow
15 Desemba 2009Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO,Anders Fogh Rasmussen anaitembelea kwa mara ya kwanza Urusi tangu alipokabidhiwa wadhifa huo Agosti mosi iliyopita.Lengo la ziara hiyo ni kurejesha hali ya kuaminiana iliyochafuliwa kufuatia vita vya Georgia,Agosti mwaka 2008.
Afghanistan itakua bila ya shaka mojawapo ya mada kuu zitakazojadiliwa wakati wa ziara hiyo,lakini waziri huyo mkuu wa zamani wa Danemark atalizusha pia suala la kinga dhidi ya makombora na mapendekezo ya Urusi ya kuwepo utaratibu mpya wa ulinzi barani Ulaya.
Wadadisi hawategemei makubwa kutokana na mazungumzo ya kesho jumatano kati ya katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO na rais wa Urusi Dmitri Medvedev na waziri mkuu Vladimir Putin.
"Uhusiano kati ya NATO na Urusi ni muhimu sana na unahitaji uangalifu,lakini hili ni suala la utaratibu" amesema hayo Andrew Monaghan,ambae ni mtaalam wa uhusiano pamoja na Urusi katika chuo cha ulinzi ncha jumuia ya kujihami ya NATO mjini Roma.
"Ni muhimu kwamba Rasmussen anakwenda Urusi na ataonana na viongozi wa nchi nhiyo,na nna hakika ziara yake italeta tija"Ameongeza kusema mtaalam huyo .
Urusi imeahidi kuchangia katika juhudi za kupambana na wataliban wa Afghanistan na balozi wake katika makao makuu ya jumuia ya kujihami ya NATO amehakikisha wiki iliyopita wako tayari kuchangia kwa kila hali,isipokua kutuma wanajeshi-miaka 20 baada ya kurejea nyumbani vikosi vya Usovieti toka Afghanistan.
Moscow inatambua kitisho cha kushindwa vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na NATO nchini Afghanistan.Matokeo yake yatakua kuwajongeza wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam jadi katika mipaka yake ya Asia ya kati.
Duru za kibalozi zinasema hata kama jumuia ya kujihami ya NATO inatambua kwanini Moscow imenyamaza kimya,hata hivyo wasingependelea kuridhika pekee na dhamiri njema zilizotangazwa na Kremlin za kuchangia zaidi katika kuwapatia vifaa wanajeshi wa Aghanistan.
Afisa mmoja wa NATO amesema jumuia hiyo ingependelea kuiona Urusi ikijitolea kuchangia helikopta zaidi kwaajili ya vikosi vya Afghanistan pamoja na bunduki na mizinga-akihoji ingekua bora silaha hizo zingetolewa kama ruzuku na sio kuuzwa.
Kipa umbele kwa NATO,amesema afisa mmoja wa ngazi ya juu wa NATO ni kuwa na uhusiano mzuri pamoja na Urusi,lakini njia bora ni kuwa na ushirikiano wa dhati badala ya majadiliano kuhusu masuala ya kifalsafa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir (AFP/Reuters)
Mhariri:Abdul-Rahman