Katibu Mkuu UN ana imani G7 zitatimiza ahadi zake
8 Oktoba 2008Mwezi uliyopita katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa nchi hizo tajiri ziliahidi kutoa kiasi cha dola billioni 16 katika mpango wa kupambana na umasikini pamoja na maradhi.
Lakini kutokana na mzozo wa fedha uliyopelekea kuyumba kwa uchumi duniani, kumekuwa na wasi wasi iwapo nchi hizo zitatimiza ahadi hiyo.
Hata hivyo Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa ana imani ahadi hizo zitatimizwa na kwamba kuna mfumo wa kuweza kufuatilia utekelezaji wa ahadi hizo.
Umoja wa Mataifa umejiwekea malengo ya kuutokomeza umasikini na njaa ifikapo mwaka 2015, ambapo Benki ya Dunia imesema kuwa watu waliyo katika umasikini uliyotopea wanaishi kwa pato la dola 1.25 kwa siku.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amesema kuwa anaunga mkono wito uliyotolewa jana na Rais wa Benki ya Dunia Robert Zoellick kutaka kuzidishwa idadi ya nchi katika kundi la G7.
Zoellick alisema nchi kama, China, India, Urusi, Saudi Arabia, Brazil, Mexico na Afrika Kusini ni lazima ziingizwe katika kundi hilo la nchi tajiri kiviwanda duniani.