Katiba mpya ya Somalia kutoa haki zaidi
27 Julai 2012Hatua ya kujumuisha haki ya kutoa mimba kwenye katiba imewafanya baadhi ya wanawake wa Somalia kuifurahia katiba mpya huku wengine wenye msimamo mkali wa kihafidhina wakitoa malalamiko juu ya kuwepo kwa haki kama hiyo. Lakini haki nyingine ambazo sasa zimeingizwa katika katiba mpya, kama vile haki ya kupata huduma ya afya na maji safi na salama, zitakuwa ngumu sana kwa serikali kutimiza. Hii ni kwa sababu hata mahitaji ya msingi kama vile chakula hayawafikii raia wote wa Somalia. Mbali na hayo, sheria ya kukataza kabisa ukeketaji kwa wasichana na wanawake itakuwa ngumu sana kufuatwa katika nchi ambayo Umoja wa Mataifa unaarifu kwamba asilimia 95 ya wanawake wamekeketwa.
Ipo pia sheria inayosema kwamba hakuna mtoto atakayeruhusiwa kufanya kazi ambayo haiendani na umri wa mtoto lakini itakuwa ngumu kufuata kwani Somalia ni nchi ambapo idadi kubwa ya watoto wanalazimika kufanya kazi. Rasimu ya katiba inasema pia kwamba kila mtoto anapaswa kulindwa dhidi ya mgogoro wa kutumia silaha lakini Somalia ni nchi yenye historia ya kuwatumia watoto kama wapiganaji na hilo limekuwa likifanywa na serikali pamoja na waasi.
Sheria ya Kiislamu ni msingi wa katiba
Viongozi 825 wa Somalia, Jumatano walianza mkutano wao wa siku 9 kuchunguza, kujadili na hatimaye kupitisha katiba ambayo imechukua miaka kadhaa kukamilika. Kipindi cha shughuli za uangalizi za Umoja wa Mataifa nchini Somalia kinakwisha tarehe 20 mwezi Agosti. Kabla ya kuisha kwa kipindi hicho, Wasomali wanapaswa kupitisha katiba mpya, kuchagua bunge jipya lenye wawakilishi 275 na vile vile kumchagua rais mpya wa kuongoza nchi hiyo.
Waziri Mkuu wa Somalia, Abdiwali Mohammed Ali, ameuita mkutano wa viongozi wa nchi yake hatua muhimu na kuongezea kwamba katiba mpya itakuwa ishara ya haki na usawa kwa ajili ya raia wa nchi yake. Hata hivyo ameeleza kwamba katiba hiyo itakuwa ya muda tu na kwamba lengo ni kupitisha katiba itakayopigiwa kura na raia wote. Hali ya usalama, uhaba wa fedha na ukosefu wa utaratibu maalum vinazuia katiba kupigiwa kura kwa sasa. Zoezi hilo huenda likafanyika miaka kadhaa baadaye. Kikundi cha kimataifa cha masuala ya sheria kimeeleza kwamba rasimu ya katiba hiyo inatoa haki nyingi za msingi kuliko hata katiba ya Marekani.
Katiba inayotumika Somalia sasa iliandikwa mwaka 2004. Katiba hiyo pia iliandikwa kama katiba ya muda tu na inatoa haki chache ikilinganishwa na rasimu ya katiba iliyoandikwa sasa. Rasimu hiyo inaweka wazi kwamba sheria ya Kiislamu ndiyo msingi wa sheria za Somalia. Ingawa imetajwa kwamba kila mtu ana haki ya kufuata dini aitakayo, hakuna dini inayoruhusiwa zaidi ya dini ya Kiislamu.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/ap
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman