1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kashfa ya upelelezi yazidi kuhanikiza

12 Agosti 2013

Kisa cha upelelezi na jinsi rais Barak Obama wa Marekani anavyojaribu kuwatuliza walimwengu pamoja pia na kampeni za uchaguzi nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini.

https://p.dw.com/p/19O0B
Kitambulisho cha mkakati wa upelelezi wa Marekani PRISMPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie lakini na kashfa kubwa kabisa ya upelelezi inayoendelea kupandisha hasira za walimwengu.Magazeti mengi ya Ujerumani yameimulika hotuba ya rais Barack Obama kuhusu umuhimu wa mageuzi katika shughuli za mashirika ya upelelezi ya NSA.Wengi wa wahariri wanasema kimsingi mageuzi yaliyopendekezwa hayatoshi. Gazeti la Kölner Stadt Anzeiger linaandika:

Kiroja hapa ni tangazo la rais Obama kwamba mashirika ya upelelezi yautumie zaidi mtandao kuzungumzia kuhusu shughuli zao ili kuimarisha hali ya kuelewana na kuaminiana pamoja na wananchi.Wamarekani kwa hivyo wanasubiri kwa hamu maelezo hayo.Mpango wa vifungu vinne wa rais Obama umelengwa kutuliza lawama za wa Marekani dhidi ya upelelezi unaofanywa na mashirika ya serikali.Hilo angalao ni la maana.Lakini mapendekezo yake ya mageuzi si chochote chengine isipokuwa hadaa.

Hoja kama hizo zimetolewa pia na gazeti la mjini Berlin la Berliner Zeitung.Ama gazeti la "Süddeutsche Zeitung" linaangalia kwa jinsi gani kashfa hiyo ya upelelezi inawaathiri wananchi wa Ujerumani.Gazeti linaendelea kuandika:

Schindler anyooshewa kidole cha shahada

Kwamba shirika la upelelezi la Marekani NSA limeziendeya kinyume kupita kiasi haki za kimsingi za wananchi wa Ujerumani,limewachunguza na kuwapeleleza-yote hayo hayamshughulishi mwenyekiti wa shirika la upelelezi la Ujerumani BND-Gerhard Schindler.Kuyapatia mashirika ya upelelezi ya Marekani data za wateja wa simu za mkono, kuuliwa watuhumiwa kwa msaada wa ndege zisizokuwa na rubani,yote hayo yanaangaliwa na uongozi wa shirika la upelelezi la Ujerumani kuwa ni jambo la kawaida.Lawama lakini zimezuka na watumishi wa shirika hilo hawakutaka tena kunyamaza na mwenyekiti akakiri kumetokea walakini.Hakubadilisha lakini kilichostahiki kubadilishwa,badala yake amethibitisha mambo yataendelea kama yalivyokuwa hadi sasa.

Kampeni za uchaguzi zapamba moto

Mada yetu ya mwisho inaturejesha hapa hapa Ujerumani ambako homa ya uchaguzi mkuu,inazidi kupanda.Karata zinachangaywa na mikakati kufikiriwa kuhusu chama kipi kiungane na kipi kuunda serikali ya muungano matokeo ya uchaguzi yatakapotangazwa?Gazeti la "Pforzheimer Zeitung" linaandika:

Kwamba wiki sita kabla ya uchaguzi mkuu,mazungumzo yanatuwama juu ya nani hatoungana na nani-ni jambo la kawaida.Vyama vya kisiasa havitaki kuwatisha wafuasi wao kwa kuashiria juu ya aina ya muungano.Mfano bayana hapa ni ule wa walinzi wa mazingira wanaosema mwanya unaowatenganisha na CDU unaazidi kupanuka.Pengine ni kweli ikizingatiwa mipango yao ya kutaka ianzishwe kodi kwaajili ya usafi wa mazingira.Lakini muungano si ndowa ya mapenzi,bali ushirikiano wa muda uliolengwa kimaslahi.Kila mmoja anameza kidonge chake.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu