1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Karzai azindua Baraza Kuu la Amani Afghanistan

7 Oktoba 2010

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan hii leo amezindua baraza la amani litakalo kuwa mpatanishi katika jitahada za kumaliza vita nchini humo.

https://p.dw.com/p/PYkF
Afghan President Hamid Karzai, center, speaks during the inaugural session of Afghanistan's new peace council, as council members Burhanuddin Rabbani, left, and Pir Sayed Ahmad Gailani, listen in Kabul, Afghanistan, Thursday, Oct. 7, 2010. Calling the meeting a "source of hope" for the Afghan people, Karzai on Thursday hosted the inaugural session of the council set up to guide efforts to reconcile with the Taliban and other insurgent groups. (AP Photo/ Gemunu Amarasinghe)
Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai akizungumza katika kikao cha kwanza cha Baraza Kuu la Amani Oktoba 07, 2010 mjini Kabul.Picha: AP

Baraza Kuu la Amani lililoundwa na Rais Karzai binafsi ni mpango wa kuanzisha mazungumzo na kundi la wanamgambo wa Taliban na waasi wengine nchini Afghanistan. Wanamgambo hao wanapigana kuipindua serikali ya Karzai tangu walipotimuliwa madarakani katika uvamizi ulioongozwa na Marekani mwishoni mwa mwaka 2001.Wataliban wameshasema waziwazi kuwa hawatofanya majadiliano yo yote na serikali mpaka wanajeshi wote wa kigeni watakapoondoka nchini humo. Hao ni wanajeshi wapatao 152,000 na wanaongozwa na Marekani.

Hata hivyo, Rais Karzai alipofungua kikao cha kwanza cha Baraza Kuu la Amani katika makao yake rasmi mjini Kabul chini ya ulinzi mkali, hakutaja kuwa leo ni miaka tisa tangu Marekani ilipoanzisha operesheni zake dhidi ya Wataliban waliokataa kuwatoa viongozi wa Al-Qaeda kuhusiana na mashambulizi ya Septemba 11. Miaka tisa baadae, Marekani inazidi kupoteza wanajeshi wake, raia wa Afghanistan wanaendelea kuuawa wakati Wataliban wakizidi kuimarika na serikali ya Afghanistan ikipoteza umaarufu kwa tuhuma za rushwa.

Kwa kweli, ripoti za mazungumzo ya siri kati ya serikali na Taliban hazikuwashtusha Waafghanistan. Kwani tangu miezi sita iliyopita pande hizo mbili zilikuwa zikifanya mazungumzo yasio rasmi. Hiyo imezusha mashaka miongoni mwa umma. Profesa Sayfuddin Sayhun wa taaluma ya siasa na uchumi katika Chuo Kikuu cha Kabul amesema:

" Ninaamini kuwa raia wa Afghanistan watakuwa wahanga wa majadiliano hayo na Taliban. Haki za kimsingi za Waafghanistan zitaathirika katika majadiliano hayo. Kwa sisi hilo sio suluhisho."

Wachambuzi wanaonya juu ya uwezekano wa kutofanikiwa kwani baraza kuu la amani limejaa wababe wa vita na viongozi wa makundi ya wanamgambo. Vile vile kuna wasiwasi miongoni mwa raia wa Afghanistan wanaoishi katika miji na hasa wale waliotajirika miaka hii tisa iliyopita. Hofu yao ni kuwa makubaliano yo yote ya kugawana madaraka na Taliban huenda yakaathiri uhuru mpya uliopatikana na hasa kuhusu wanawake. Mwanasheria na mwanaharakati wa haki za wanawake Fawzia Koofi alipozungumza na shirika la habari la AFP amesema hofu yake kubwa ni kuwa Afghanistan itarejea katika enzi ya uovu ya Wataliban ambapo wanawake hawakuheshimiwa kama binadamu.

Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post, kiongozi wa Taliban Mullah Mohammad Omar anaesemekana kuwa amejificha Pakistan, ameunga mkono majadiliano ya siri pamoja na serikali ya Afghanistan. Kuambatana na makubaliano ya majadiliano hayo mapya, viongozi wa Taliban waruhusiwe kuwa na vyeo serikalini. Vile ikubaliwe ratiba ya kuyarejesha nyumbani majeshi ya Marekani na NATO.

Mwandishi:Martin,Prema/AFPE/ZPR

Mpitiaji:Charo,Josephat