Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl afariki dunia
16 Juni 2017Aliekuwa Kansela wa Ujerumani Helmut Kohl ni mwanasiasa aliezitambua haraka alama za nyakati. Hakuchelewa kuutambua wasaa wa kuchukua hatua zilizowaunganisha tena Wajerumani.
Alipoulizwa kuhusu kujengwa mnara wa kumbukumbu wa kukumbusha juu ya kazi yake, Helmut Kohl alijibu kwa utani kwa kusema, kwamba wageni wakishaondoka, kwanza watakuja njiwa na halafu watakuja mbwa. Watakachokifanya njiwa na watakachokifanya mbwa hao kinajulikana.
Jina la Helmut Kohl lilipanda juu katika historia, kutokana na umahiri wake wa kuongoza mambo, baada ya kuanguka kwa kuta la Berlin na kuongoza hatua za kuungana tena kwa nchi mbili za kijerumani. Hayo aliyoyafanya yangetosha kumjengea mnara wa kumbumbuku.
Gharama za kuungana upya Ujerumani
Kohl alisimama safu moja na watu wengi mashuhuri duniani. Lakini kisiasa Kohl alikuwa amefikia mwisho mnamo mwaka wa kihistoria wa 1989. Wapinzani wake ndani ya chama walisimama kidete dhidi yake: ulikuwa uasi dhahiri dhidi yake.
Ni kwa taabu tu kwamba aliweza kuendelea kwa mara nyingine kuzishika hatamu za uongozi wa chama chake cha CDU. Hata katika hali mbaya ya kiafya Kohl aliweza kuonyesha ukakamavu.Yeye ni mtendaji mwenye umahiri. Ni mwanasiasa aliekuwa na uwezo wa kutangamanisha silika ya uongozi thabiti na mkakati wa utekelezaji.
Na fursa ya kuyathibitisha hayo ilijitokeza:Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani - yaani Ujerumani Mashariki ya hapo awali, ilisambaratika na kuta la Berlin liliporomoka. Helmut Kohl aliitambua fursa hiyo ya kipekee na hakuchelewa kuchukua hatua. Na alichukua hatua sahihi.
Kohl alisimama bungeni na kuuwasilisha mpango wa vipengee 10 juu ya kuungana tena kwa nchi mbili za kijerumani. Aliichukua hatua hiyo wiki tatu baada ummati wa watu kutoka Ujerumani mashariki kusongamana kwenye vituo vya kuvukia mipaka katika mji wa Berlin. Hiyo ilikuwa kazi ya umahiri mkubwa .
Hata hivyo lengo la nchi mbili za kijerumani kuungana tena lilisababisha hisia za mchanganyiko katika nchi za nje. Lakini Kohl aliwakabili wale waliokuwa na mashaka kama mwanaulaya. Kama alivyofanya pia tarahe 19 mwezi wa Desemba mjini Dresden mbele ya maalfu ya raia wa Ujerumani Mashariki. Aliutumia ulimi wa nadhari mbele ya mkutano wa hadhara wa maalfu waliokuwa na jazba- mkutano ambao haukupangwa. Na aliweza kupata imani ya watu hao.
Umahiri wake wa kisiasa
Sambamba na maandalizi ya sera ya ndani ya kuujenga umoja wa nchi mbili za kijerumani, sera ya nje ya Helmut Kohl mnamo miaka hiyo, ilithibitisha umahiri wa serikali yake. Urafiki na Ufaransa, maridhiano na Poland na uhusiano katika msingi wa kuelewana na Urusi iliyodhoofika wakati huo, ni ishara za siasa ya makini ya Kohl kwa nchi jirani.
Helmut Kohl alikuwa mtoto wakati wa vita vikuu vya pili. Alikishuhudia kipindi cha magofu nchini Ujerumani alipokuwa kijana. Na yeye alikuwa mtetezi mkubwa wa rika linaloifuata sera ya kuhakikisha kwamba vita asilani havizuki tena kutokea Ujerumani.
Ni kutokana na juhudi za mwanasiasa Kohl kwamba Ujerumani iliyoungana tena, ilirejea katika jamii ya Ulaya kuanzia mwaka wa 1990. Kohl alilitathmini bara la Ulaya kuwa ni jukumu la Ujerumani. Na kwa ajili hiyo aliipigania sarafu ya Euro kwa nguvu zake zote, kwa lengo la kuhakikisha kwamba mchakato wa kuujenga Umoja wa Ulaya haurudi nyuma. Aliweka shinikizo ili nchi za Ulaya Mashariki ziingizwe katika Umoja huo, licha ya changamoto kubwa kwa jumuiya.
Helmut Kohl ataendelea kukumbukwa
Yeye siyo sawa na Willy Brandt, mwanasiasa aliekuwa na uwezo wa kuona mbali na wala yeye hawezi kufananishwa na Helmut Schmidt, mtaalamu wa uchumi. Kohl alikuwa Mjerumani lakini zaidi alikuwa mwanaulaya mkubwa.
Kohl alikuwa kansela aliyekaa muda mrefu zaidi madarakani baada ya Vita vya Pili vya Dunia, akihudumu kutoka mwaka 1982 hadi 1998 na akihusika moja kwa moja na kuanzishwa kwa sarafu ya pamoja ya bara la Ulaya, Euro.
Mwandishi:Wagener, Volker
Mfasiriri:Mtullya Abdu.
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman