Kansela wa zamani wa Austria Sebastian Kurz atiwa hatiani
24 Februari 2024Mahakama ya mjini Vienna imemkuta na hatia kansela wa zamani wa Austria Sebastian Kurz kwa kosa la kutoa ushahidi wa uongo katika uchunguzi wa bunge na kumuhukumu kifungo cha miezi minane jela kilichosimamishwa.
Hukumu hiyo ya jana Ijumaa ilitolewa mwishoni mwa kesi iliyokuwa ikisikilizwa kwa miezi kadhaa dhidi ya mwanasiasa huyo wa zamani ambaye aliwahi kupongezwa kama mwanasiasa mwenye umri mdogo aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kushangaza miongoni mwa mahafidhina wa Ulaya.
Kurz, mwenye umri wa miaka 37, amesema atakata rufaa akiieleza hukumu dhidi yake kuwa ya kushaganza na isiyo ya haki.
Kurz alihukumiwa kwa kupotosha uchunguzi wa bunge kuhusu kashfa mbalimbali za rushwa ambazo ziliiangusha serikali yake ya kwanza ya mseto na chama cha mrengo mkali wa kulia mnamo 2019.