Kansela wa Ujerumani yu ziarani Japan
29 Agosti 2007Mazungumzo yake huko, kama ilivokuwa Uchina, yatahusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani na ulinzi wa mazingira. Mwisho wa mwaka huu, Japan itachukuwa nafasi ya Ujerumani kuwa mwenyekiti wa kundi la nchi nane zinazoongoza kiviwanda duniani. Ziara hii ya Bibi Merkel basi ni kama aina ya kukabidhiana wadhifa.
Hata ikiwa kwa mtazamo wa Ujerumani, Uchina na Japan zinakaribiana, kuichanganyisha ziara ya Uchina pamoja na ya Japan kwa sababu ya kukaribiana nchi hizo mbili, kijiografia, kunatoa hisia iliokuwa si nzuri kwa nchi hizo mbili za Asia. Sababu ni kwamba Uchina na Japan kwa sasa ziko katika mashindano ya kujionesha na kutaka kupata ushawishi duniani. Kwa hivyo huko Peking watu wamekasirika kwamba Kansela Merkel baada ya kuondoka mji huo ameelekea Japan.
Ule mpango wa mwanzo wa Wajerumani kwamba ziara jiyo ianzie Japan kwanza ulikataliwa katukatu na upande wa Wachina. Katika sarakasi hii ya kuonesha misuli ya kidiplomasia, Japan haijataka kuburuzwa. Serekali ya Japan ilimuoneshea kansela namna inavomthamini sana kwa kuiweka ziara yake, japokuwa si kwa njia rasmi ya kiitifaki, katika daraja ya juu zaidi kuliko ile iliofanywa na mtangulizi wake, Gerhard Schroader, karibu miaka mitatu iliopita.
Leo Bibi Merkel amepokewa na kusindikizwa na gari za polisi kupitia kwenye msongamano wa magari katikati ya mji mkuu wa Japan hadi akawasili katika makao makuu ya waziri mkuu Shinzo Abe. Kinyume na yaliompata mtangulizi wake, Gerhard Schroader, pale alipokwama pamoja na mlolongo wa magari yaliokuwa yakimsindikiza katika msongamano wa magari katikati ya daraja mjini Tokyo.
Mkutano wake na mwenzake wa Japan utakuwa kama kukabidhiana wadhifa, kwani Japan mwakani itakamata kutoka Ujerumani uwenyekiti wa kundi la nchi nane zinazoongoza kiviwanda duniani. Kansela anataka Japan iuendeleze ule mradi aliouanzisha, nao ni pamoja na kupunguza moshi katika hewa na kujenga ushirikiano wa karibu zaidi baina ya nchi za viwanda na zile muhimu zinaoinukia, zoezi lililopewa jina la Mwenendo wa Heiligendamm.
Kinyume na Ujerumani, Japan haitoweka malengo ya kufikiwa kwa haraka juu ya ulinzi wa hali ya hewa, lakini kwanza itaziwajibisha Uchina na India juu ya suala la kuhifadhi hewa safi. Bila ya kushiriki nchi mbili hizo ambazo ni watoaji wakubwa wa moshi mchafu hewani, hakutafikiwa kile kiwango kilichowekwa cha uchafu katika hewa. Japan inasema vinu vya kinyukliya ni dawa katika kupambana na ujoto duniani.
Lakini katika makala iliochapishwa katika ukurasa wa mbele wa gazeti la kiliberali la Asashi huko Japan, Ujerumani imesifiwa kwa kuwa mbele katika kupigania usafi wa hali ya hewa. Akiwa kama waziri wa mazingira miaka 10 iliopita, Bibi Merkel alishiriki katika mashauriano yaliopelekea kupatikana Itifaki ya Tokyo. Na sasa, kama kansela, ameweka malengo kwa nchi yake ili kutekeleza yale yaliotakiwa na Itifaki hiyo.
Licha ya masuala ya hali ya hewa duniani, ziara ya Kansela huko Japan pia itatwama juu ya ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo mbili. Hivi sasa Ujerumani ni nchi muhimu kwa uwekezaji kwa makampuni ya Kijapani. Upungufu wa ajabu katika ziara hii ya kiserekali ya Bibi Merkel! Nao ni kwamba japokuwa
Kansela analiwekea uzito mkubwa suala la utundu katika uvúmbuzi, mada hiyo itakuwa na umuhimu tu wakati atakapokula chakula cha mchana na wanasayansi wa Kijapani. Katika jambo hilo, Ujerumani inaweza kusoma kutoka Japan Viwanda na serekali katika Japan vinatoa fedha mara mbili zaidi kuliko inavotoa Ujerumani kwa ajili ya utafiti na utengenezaji wa bidhaa. Japan inaoongoza katika teknolojia nyingi na, kwa mujibu wa mabingwa, ni nchi ilio na utundu mkubwa kabisa katika shughuli za uvumbuzi.