1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Scholz azuru bara la Afrika

Josephat Charo
22 Mei 2022

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anafanya ziara ya kwanza barani Afrika inayoanzia nchini Senegal. Scholz anakabiliwa na kibarua kigumu katika eneo la Sahel.

https://p.dw.com/p/4BhEI
Kabinettsklausur in Meseberg
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kansela Scholz, anafanya ziara ya kwanza kabisa barani Afrika inayoanzia nchini Senegal Jumapili. Scholz anakabiliwa na kibarua kigumu na analazimika kuzingatia mabadiliko ya mahusiano ya madaraka katika eneo la Sahel. Wachambuzi wanatarajia ahadi za wazi na uongozi mpya kuchukua nafasi ya Ufaransa. Ni ziara inayonuiwa kuhakikisha muendelezo katika kipindi kigumu. Scholz atazitembelea pia Niger na Afrika Kusini.

Ziara ya Scholz Afrika Maghribi inahusu kusisitiza ushirikiano wa kimkakati pande zote za Mali, ambayo maamuzi yake ya hivi karibuni yamesababisha nchi hiyo kutengwa na washirika wake wa Ulaya. Senegal, ambayo inashikilia urais wa Umoja wa Afrika, ni mshirika wa kundi la nchi saba tajiri zilizostawi kiviwanda duniani za G7. Niger, kama mshirika wa kijeshi na nchi inayotumiwa kama njia ya wahamiaji wanaoeleka Ulaya, imekuwa na umuhimu mkubwa kwa kipindi kirefu katika mikakati ya Ulaya barani Afrika.

Mtaalamu wa masuala ya usalama Priya Singh wa taasisi ya masomo kuhusu usalama ISS, nchini Afrika Kusini, anasema Ujerumani haipeleki mzigo kama ule wa Ufaransa katika eneo la Sahel. Mpaka siku za hivi karibuni, Ufaransa, mkoloni wa zamani wa Senegal, ilikoselewa mara kwa mara kwa kufuatilia ajenda yake Afrika Magharibi, na watu wa Niger pia walijimwaga mabarabarani na ujumbe wa kuipinga Ufaransa.

Singh ameiambia DW katika mahojiano kwamba Ujerumani huenda ikawa mshirika asiyeegemea upande wowote kuliko Ufaransa, kwa sababu mpaka sasa imejikita na kuelekeza nguvu katika mahusiano ya kiuchumi.

Operation Barkhane in Mali
Picha: Philippe De Poulpiquet/MAXPPP/dpa/picture alliance

Hata hivyo kwa upande mwingine umma wa Senegal una wasiwasi kuhusu wanajeshi wa kimataifa kuendelea kukaa nchini mwao. Hili linasisitizwa na Olaf Bernau, mwanachama wa kamati ya mtandao wa mashirika ya kijamii hapa Ujerumani, Fokus Sahel. Akizungumza na DW Bernau amesema wakati wa mazungumzo ya mtandao wake na watu wa Niger, hofu kwamba wanajeshi wa kigeni huenda wakaupeleka mzozo na makundi ya wapiganaji wa jihad hadi katika nchi hiyo ya eneo la Sahel ipo. Amesema ujumbe kutoka kwa kansela Scholz unaweza tu kuwa ombi la kuishawishi Ufaransa isiwatume tena wanajeshi wake nchini Niger.

Matumaini ya ziara ya Scholz Afrika ni makubwa

Ujerumani imekuwa ikitoa mafunzo kwa vikosi maalumu vya Niger katika operesheni ya kijeshi "Operation Gazelle" tangu mwaka 2018. Operesheni hiyo, ambayo inatarajiwa kukamilika mwisho wa mwaka huu, inapongezwa na wizara ya ulinzi kama mfano uliofanikiwa wa ushirikiano wa kimataifa wa usalama unaoweza kuhamishwa na kuigwa katika nchi nyingine.

Wajumbe wa biashara wana matumaini makubwa kuhusu ziara ya kansela Scholz. Volker Treier, Mkuu wa masuala ya baishara katika nchi za kigeni katika chemba ya viwanda na biashara ya Ujerumani anasema ziara hiyo inafanyika wakati muafaka. Akizungumza na DW, Treier amesema vita vya Urusi nchini Ukraine, pamoja na kufungwa kwa shughuli mjini Shanghai na maeneo ya China, kumedhihirisha utegemezi katika sekta ya nishati. Amesisitiza kwamba tunahitaji kubadilishana na kushirikiana na nchi nyingine katika njia nyingi, kukamilisha mikataba ya masuala ya nishati na pia usalama.

Katika maeneo haya Afrika inaipa Ujerumani mitazamo muhimu, na sio tu kuhusu nishati inayotokana na vitu asili kama gesi. Senegal imewekeza sana katika nishati inayotokana na jua katika miaka ya hivi karibuni na huenda ikawa na jukumu muhimu kwa kuanzia. Treier ana imani kwamba kansela Scholz anatuma ujumbe sahihi, anaweka wazi kwamba linapokuja suala la nchi za kiafrika, hatuwezi tu kudai. Tunalazimika pia kutoa kitu.

Ziara ya Scholz inafanyika baada ya rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier kulazimika kukatiza ziara yake Senegal mwezi Februari.

Phillip Sandner/DW