1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel:Tusiitegemee Marekani katika NATO

Jane Nyingi
13 Januari 2017

Kansela wa Ujerumani  Angela Merkel ametoa wito  kwa wanachama wa umoja wa ulaya kuimarisha ushirikano wao katika swala la usalama na ulinzi kutokana na kutokuwepo hakikisho la kudumu katika mahusiano yao na Marekani.

https://p.dw.com/p/2Vkh9
Luxemburg Besuch Angela Merkel
Picha: picture-alliance/dpa/H. Tittel

Umoja huo unakabiliwa na  changamoto zinazozidi kuongezeka katika mipaka yake na maeneo  jirani ikiwa ni pamoja na uhamiaji, ongezeko la vitisho vya ugaidi, vita nchini Syria, vurugu mashariki mwa Ukraine na umaskini na njaa barani Afrika. 

Japo Kansela Merkel hamkutaja Rais mteule Donald Trump kwa jina wakati akieleza changamoto hizo, ilikuwa bayana alikuwa akiyalenga matamshi aliyoyatoa Trump wakati wa kampeini zake kuwa atafikiria upya mchango wa Marekani katika Jumuiya ya NATO kabla ya kutoa msaada wowote.Trump pia aliutaja ushirika huo wa kijeshi wa mataifa ya magharibi kama uliopitwa na wakati.
"Dunia inayokabiliwa na misukosuko,migogoro ya mara kwa mara,mashambulizi ya mitandaoni, hizi  ni baadhi ya changomoto  zinazotukabili sisi sote. Kwa hivyo ni muhimu kuchukua hatua kwa pamoja.Na ni wazi,na Ujerumani inafahamu hilo,kuwa  tunahitaji  kutumia fedha zaidi  ili bara la Ulaya  litimize wajibu wake wa kimataifa  sio tu ndani ya NATO bali pia ndani ya Umoja wa Ulaya” alisema Merkel

Nato-Übung Dragon-15 Bundeswehr Polen
Wanajeshi wa Ujerumani walio katika muungano wa NATOPicha: picture-alliance/dpa/T. Waszcuk

Mwezi Novemba mwaka uliopita Kansela Merkel alisema Ujerumani  lazima  iongeze  kiwango cha fedha inachotumia katika ulinzi ili kufikia malengo ya jumuiya ya NATO ya asilimia 2 ya pato la taifa, lakini akapuuzilia mbali matarajio kuwa malengo hayo yatatimizwa katika siku za hivi karibuni.

Umoja wa Ulaya  ambao umekuwa ukiitegemea Marekani kuuhakikisha usalama wake katika kipindi cha miongo saba,ulikubali kuchukua hatua  kuelekea kuimarisha ushirikiano wao wa usalama na ulinzi  katika mkutano wa kilele uliofanyika mwezi Disemba. Merkel ambae pia amekosolewa hapa Ujerumani kutokana na sera yake ya milango wazi kwa wakimbizi, pia aliutaka umoja wa ulaya kuharakisha  kazi yake katika sajili ya kuingia na kutoka ili kutoa ulinzi unaohitajika mipakani. Kuhusu Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya Kansela Merkel aliwataka wanachama 27 wa Umoja huo waliosalia kuzungumza kwa sauti moja."Kuhusu Brexit, ambayo sisi pia tulizungumzia, ni muhimu kutoruhusu kugawanywa .Lazima tukae meza ya mazungumzo  kwa pamoja kama wanachama 27. Lakini  kwanza  lazima tusubiri majibu  kutoka kwa Uingereza inavyotaka  kutekeleza Brexit"

Großbritannien Brexit-Proteste
Waandamanaji waliounga mkono BrexitPicha: REUTERS/T. Melville

Waingereza walipiga kura mwezi Juni mwaka jana kuondoka EU lakini wanachama wa Umoja huo wamekataa kushiriki mazungumzo yoyote kuhusu uhusino wao wa baadae  na Uingereza hadi kutekelezwa kipengee cha 50  cha kujiondoa katika Umoja huo.

 

Mwandishi:Jane Nyingi/AFP/RTRE
Mhariri:Iddi Ssessanga