1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel: Shambulio la Berlin ni ugaidi

Admin.WagnerD20 Desemba 2016

Polisi imesema inayo tashwishi ikiwa kweli raia wa Pakistan wanayemzulia ndiye aliliendesha lori kwenye kusanyiko la watu na kuwaua watu 12 na wengine 50 kujeruhiwa.

https://p.dw.com/p/2UcHi
Deutschland Merkel Statement zum Anschlag in Berlin
Picha: Reuters/H. Hanschke

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema anachukuliwa tukio la lori kuparamiya soko la Krismas mjini Berlin na kuuwa watu 12 kuwa la kigaidi, huku maafisa wakieleza mashaka juu ya iwapo mshukiwa wa shambulizi hilo waliemkamata ndiye mtu sahihi. 

Kansela Angela Merkel aliyejieleza kuwa ameshangazwa, ametetemeshwa na kuhuzunishwa na mkasa huo, amesema Ujerumani laazima ilichukulie shambulizi hilo kuwa la kigaidi, na kuahidi kuwa wahusika watakabiliwa kikamilifu na mkono wa sheria.

''Ninayo imani kubwa kwa wachunguzi wa mkasa huu wa kihayawani na ninaamini utasuluhishwa kwa kila hatua na wahusika wataadhibiwa vikali kufuatana na sheria zetu. Kuna mambo mengi ambayo bado hatujui kwa uhakika lakini kwa sasa tunalichukulia kuwa shambulio la kigaidi.''

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amethibitisha kwamba mkasa huo uliofanyika katika soko maalum la Krismasi mjini Berlin ulikuwa shambulio lililokusudiwa. Akizungumza baada ya kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambp ya ndani wa majimbo, de Maiziere amesema kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS halijadai kuhusika. ''Kwa sasa hatuna tashwishi yoyote kuwa mkasa huu mbaya uliotokea usiku ulikuwa shambulio. Lori liliendeshwa kwa makusudi kuelekea kwa watu walionuia kuwa na jioni njema katika soko la Krismasi''.

Eneo la shambulio
Eneo la shambulioPicha: Reuters/C. Mang

Huenda mtuhumiwa anayezuliwa na polisi si mhusika

Tofauti na walivyodokeza hapo awali kuhusu mtuhumiwa wa shambulio hilo, iIdara ya polisi Ujerumani sasa imesema kuna tashwishi kama kweli raia wa Pakistan anayeshikiliwa kwa kushukiwa kuhusika ndiye aliliendesha lori lile lililosababisha vifo vya watu 12 na kuwajeruhi wengine 50.  Mshukiwa huyo aliyeomba uhifadhi nchini Ujerumani mwezi Disemba mwaka jana na kuwasili jijini Berlin mwezi Februari, amekana kuhusika na kisa hicho.

Viongozi mbalimbali akiwemo rais Francois Hollande wa Ufaransa wametuma risala zao kufuatia shambulio hilo. Polisi imesema itaimarisha usalama zaidi katika masoko hayo maalum ya Krismasi ikiwemo kuweka vizuizi madhubuti. imetaka wakaazi wa Berlin kuwa macho hasa ikizingatiwa mshukiwa mkuu hajatambuliwa wazi.

Mwandishi: John Juma/DPE/APE/

Mhariri: Iddi Ssessanga