Kansela Merkel kukutana na Youssef Chahed wa Tunisia
14 Februari 2017Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajiwa kumshinikiza waziri mkuu wa Tunisia Youssef Chahed kuharakisha kurejeshwa nyumbani kwa watu waliokuwa wanatafuta hifadhi. Bw Chahed yuko ziarani mjini Berlin.
Suala hilo limekuwa la dharura kwa Ujerumani tangu lile shambulizi la kigaidi katika soko la Krismasi Desemba iliyopita, linalodaiwa kutekelezwa na raia wa Tunisia Anis Amri, aliyestahili kurejeshwa nchini mwake miezi michache iliyopita.
Baada ya shambulizi hilo lililopelekea vifo vya watu 12, ilibainika kwamba ombi la Amri la kutaka hifadhi lilikataliwa nusu mwaka kabla, ingawa hakuwezya kurejeshwa nchini mwake kutokana na ajizi iliyotokana na sheria za nchini Tunisia.
Katika ujumbe alioutoa siku ya Jumamosi Merkel alisema watunisia waliokataliwa maombi ya hifadhi ni sharti warejeshwe kwao haraka iwezekanavyo.
Ujerumani katika hali ngumu ya kukabiliana na wakimbizi wengi
Kiongozi huyo wa Ujerumani ameahidi kulijadili suala hilo na waziri mkuu Chahed akisema kwamba ni sharti lizingatiwe hasa iwapo kuna tishio la usalama wa umma.
Ujerumani imejipata katika hali ngumu ya kukabiliana na tatizo la wahamiaji tangu mwaka wa 2015, pale Merkel alipoanzisha sera ya kuwakubalia wakimbizi kuingia nchini humo bila vikwazo, kutoka mataifa yenye mizozo kama Syria na Afghanistan.
Ongezeko la wahamiaji nchini Ujerumani lilizua maswali kuhusiana na shinikizo litakalokuwa kwenye miundo msingi na tishio la usalama, jambo lililowapelekea wengi kupinga suala hilo la uhamiaji.
Huku ikiwa maombi ya kutaka hifadhi ya wakimbizi wengi kutoka Syria, taifa linalokabiliwa na vita yamakubaliwa, yale maombi kutoka Tunisia, Algeria na Morocco yamekataliwa kwa kuwa nchi zao zinadaiwa kuwa imara.
Ujerumani inahofia wahamiaji kuanza kuinga tena Ulaya
Merkel amesisitiza kwamba anataka Ujerumani kuziorodhesha Tunisia, Morocco na Algeria kama nchi salama, suala litakalozidisha ugumu wa wanaotafuta uhifadhi kukubaliwa, ingawa pendekezo lake halijapitishwa katika bungeni mjini Berlin kutokana na madai ya kulindwa kwa haki za kibinadamu.
Ujerumani ambayo imekua nchi inayowapokea wakimbizi kwawingi katika miaka ya hivi majuzi, inahofia kwamba kutakuwa na ongezeko la wahamiaji wanaovuka bahari ya Mediterenia kuingia nchini humu mara msimu wa baridi utakapokwisha.
Lakini Ujerumani inataraji kwamba mataifa mengine katika kanda ya Ulaya yataisaidia katika kuwazuia wakimbizi wasiingie katika eneo la umoja wa ulaya EU.
Mwaka wa 2016, watu 55,000 walirejea kwa hiari katika mataifa yao kutoka Ujerumani, huku wengine 25,000 wakifurushwa. lakini mwishoni mwa mwaka huo, watu 200,000 waliotakiwa kuondoka, walisalia Ujerumani 54,000 kati yao walinyimwa vibali kubakia zaidi.
Kansela Merkel lakini ameitaja Tunisia kuwa mhimili matumaini na amezungumzia suala la kuipa msaada wa maendeleo, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya kazi vijana ili kupunguza kiwango kikubwa cha wasio na ajira.
Mwandishi: Jacob Safarri/DPA/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman