1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel Afghanistan

Wanjiku Schulte/ Küstner Kai6 Aprili 2009

Kambi ya jeshi la Ujerumani Kundus yashambuliwa kwa roketi

https://p.dw.com/p/HRRD
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akizungumza na wanajeshi wa Ujerumani huko KunduzPicha: AP

Muda mfupi baada ya ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merekel ambayo ilikuwa haijatangazwa rasmi, kambi ya kikosi cha Ujerumani huko Kundsuz kaskazini mwa Afghanistan kilishambuliwa na roketi. Kansela Merkel alikuwa ameondoka dakika ishirini kabla ya shambulio hilo akielekea Masar-i- Sharif amesema msemaji wa serikali Thomas Steg hii leo akiwa mjini Berlin. Kwa mujibu wa waziri wa ulinzi roketi hizo mbili ziligonga nje ya kambi na hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Kansela Angela Merkel amechagua kukitembelea kituo cha jeshi la Ujerumani kinachokabiliwa na hatari kubwa. Akiandamana na waziri wa ulinzi Franz-Josef Jung ,Kansela Merkel amekitembelea kituo hicho chenye timu ya wajenzi wanaohusika na shughuli za kuijenga upya Afghanistan huko Kundus.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kwenye mtandao wa jeshi hilo kambi hiyo imeshambuliwa kwa roketi leo asubuhi. Msemaji wa serekali amethibitisha kwamba roketi hizo mbili ziliikosa kambi hio dakika 20 baada ya Kansela Merkel kuondoka mahali hapo. Hata hivyo hii inaonyesha vile hali ilivyo mbaya huko Kundus. Miaka iliyopita kambi hiyo ilishambuliwa karibu mara 20 ambapo katika mashambulizi hayo wanajeshi watatu wa Ujerumani waliuwawa.

Ni dhahiri kwamba wakati huu Kansela Merkel alikuwa amechagua kujionea eneo la kaskazini mwa Afghanistan pekee, yaani sehemu ambayo majeshi ya Ujerumani yana kambi zao. Mji mkuu Kabul ulikuwa hauko katika mipango ya safari ya Kansela Merkel na kumhusu rais Hamid Karzai, ilibidi atosheke na mazungumzo kwa njia simu.

Kansela Merkel alizuru Afghanistan Novemba mwaka wa 2007 mara ya mwisho, na hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kabisa na wakati huo walinzi wake walimshauri avae mavazi ya kumkinga kutokana na risasi.

Barabara hatari kabisa huko mjini Kabul alizunguka mjini humo kwa kutumia helikopta. Hata wakati huu ziara yake inafanyika chini ya ulinzi mkali, hata mpaka dakika ya mwisho ziara ya Bi Merkel ilikuwa ni siri.

Lengo la ziara ya Merkel

Madhumuni ya ziara hii inayofanyika muda mfupi baada ya mkutano wa jumuiya ya kujihami ya NATO kumalizika ilitarajiwa kuonyesha ulimwengu kwamba Ujerumani pia inajali hali ilivyo huko Afghanistan. Wakati huo huo Kansela Merkel hangetaka kunyoshewa kidole cha lawama katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu, kuwa aliitembelea Afghanistan mara moja tu wakati akiwa mamlakani. Kwani mgombea ukansela wa Ujerumani katika uchaguzi ujao Bwana Frank Walter Steinmeier aliwahi kuitembelea nchi hiyo mwaka uliopita.

Aussenminister Steinmeier Rede zum Wahlsieg Barack Obama
Naibu kansela wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: AP

Mwishoni mwa wiki iliyopita jumuiya ya kujihami ya NATO ilikubaliana juu ya kuweka mikakati mipya juu ya Afghanistan. Majeshi na fedha zaidi ndivyo vipengele viwili muhimu vilivyopitishwa katika mpango huo. Marekani inataka kutuma majeshi 21,000 zaidi na Kansela Merkel amesema pia Ujerumani itatuma majeshi 600 zaidi ili kuimarisha nafasi yake ya kushinda uchaguzi wa Ujerumani mwezi wa Agosti mwaka huu.

Mwaka jana wakati wa majira ya mapukutiko bunge la Ujerumani liliweka idadi ya wanajeshi 4500 kama kiwango cha juu kitakachotumwa Afghanistan.