Kansela Merkel atoa tamko la serikali
18 Oktoba 2012Kansela Merkel ameyasema hayo muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Akizungumza Bungeni mjini Berlin, kutoa tamko la serikali, Kansela Merkel pia ametoa mwito wa kuleta ustawi zaidi. Akisisitiza umuhimu wa sarafu ya Euro, Kansela wa Ujerumani amesema kuwa "Sarafu ya Euro, siyo fedha tu." Amesema Euro ni ishara hai ya umoja wa Ulaya kisiasa, kiuchumi na kijamii na kwamba ina uzito pia nje ya bara la Ulaya.
Katika tamko la serikali alilolitoa bungeni, Kansela Merkel pia amesifu juhudi zilizofanyika hadi sasa katika kukabiliana na mgogoro wa Euro na ametoa mwito wa kuanzisha mifuko mipya ili kuzisaidia serikali zilizolemewa na madeni ili ziweze kufadhili miradi maalamu. Ameeleza kuwa kwa njia hiyo itawezakana kuanzisha kigezo kipya cha mshikamano katika juhudi za kupambana na mgogoro wa madeni.
Merkel aunga mkono pendekezo
Katika tamko lake Kansela Merkel pia ameunga mkono pendekezo la kuipa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya mamlaka juu ya bajeti za nchi wanachama za Umoja wa sarafu ya Euro. Bibi Merkel pia amesema juhudi za kuukabili mgogoro wa Euro zitaaendelea kufanywa hata baada ya mkutano wa mjini Brussels. Amesema mikutano mingine itafuatia.
Kansela Merkel amesema anapendelea sana kuona kwamba Ugiriki inaendelea kuwamo katika Umoja wa sarafu ya Euro kwa sababu amesema, pamoja na kuwa rafiki na mshirika wa jumuiya ya kujihami ya NATO, Ugiriki ni sehemu ya Ulaya. Lakini bibi Merkel ameshutumu rushwa nchini Ugiriki. Kiongozi huyo wa Ujerumani kwa mara nyingine amepinga wazo la kuyaleta pamoja madeni ya nchi zote ili yalipwe na nchi zote.
Akizunguma kujibu tamko la serikali mjumbe atakayegombea ukansela kwa tiketi ya chama kikuu cha upinzani, SPD, Bwana Peer Steinbrück, amemlaumu Kansela Merkel kwa undumakuwili katika juhudi za kupambana na mgogoro wa madeni. Amemtaka Kansela Merkel aseme kwamba, kuhusu Ugiriki, Ujerumani inapaswa kutimiza wajibu zaidi kwa kushirikiana na nchi nyingine.
Mkutano wa kilele wa viongozi kutoka nchi 27 za Umoja wa Ulaya mjini Brussels utajadili mustakabali wa sarafu ya Euro na njia za kuondokana na mgogoro wa madeni.
Mwandishi: Mtullya Abdu/dpae, ZA
Mhariri: Josephat Charo