Kansela Merkel atetea makubaliano na Iran bungeni
16 Mei 2018Katika hotuba yake iliyogusia mambo mbali mbali katika bunge la Ujerumani Bundestag , kansela Merkel amezungumzia masuala kadhaa kuanzia mageuzi ya msingi kabisa hadi ulinzi na hatua za kidigitali,bila hata hivyo kuelezea undani mkakati wa mipango hiyo.
Mtazamo wenye ncha nyingi, ikiwa ni pamoja na kuielekea Iran , ni njia pekee, amesema Merkel, ambaye pamoja na mataifa mengine ya Ulaya yanajaribu kuyanusuru makubaliano hayo ya kinyuklia bila ya Marekani.
Merkel ameyaeleza makubaliano hayo kuwa nsio kamilifu, lakini akaongeza kwamba maafisa wa kimataifa wanaohusika na masuala ya kinyuklia wamesema Iran inatekeleza majukumu yake.
"Hii haina maana kwamba tunafurahia kila kitu ambacho Iran inafanya , tunapaswa kuzungumzia juu ya kujihusisha kwa Iran nchini Syria , mpango wake wa makombora, na masuala mengine, lakini swali iwapo unaweza kufanikiwa zaidi ikiwa utasitisha makubaliano ama iwapo unakaa nje ya makubaliano hayo," Merkel amewaambia wabunge leo.
"tunasema unaweza kuzungumza vizuri zaidi iwapo utabakia katika makubaliano," aliongeza Merkel.
Uhusiano kati ya Ulaya na Marekani
Wiki iliyopita, rais wa Marekani Donald Trump alijitoa katika makubaliano ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani ambayo yaliondoa vikwazo vya kiuchumi vingi vya kimataifa ili Iran iweze kusitisha mpango wake wa kinyuklia, ukiwa chini ya uangalizi wa shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia nishati ya atomiki.
Katika hotuba yake Merkel amedokeza kwamba licha ya kuwapo na matatizo hivi sasa, uhusiano wa mataifa ya Ulaya na Marekani utabakia kuwa muhimu. Lakini pia alitoa tahadhari.
"Lakini uhusiano huu wa mataifa yanayopakana na bahari ya Atlantic pia ni lazima uwe na uwezo wa kuhimili tofauti ya mawazo, hususan kama tunavyoona siku hizi kwa Marekani kujitoa kutoka katika makubaliano ya kinyuklia na Iran."
Merkel pia alitoa wito wa kuimarishwa kwa kanda ya sarafu ya euro na kuweka uzito katika pendekezo kutoka kwa waziri wake wa fedha kutoka chama cha Social democratic SPD, Olaf Scholz kuubadilisha mfuko wa Ulaya wa mfumo wa kuleta uthabiti ESM, na kuwa chombo kitakachotumika kukamilisha kufungwa kwa mabenki yanayofanya vibaya.
Merkel na Scholz wanatofautiana na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusiana na mawazo yake ya msimamo mkali ya kuweka bajeti maalumu ya mataifa ya kanda ya sarafu ya euro, na kumteua waziri wa fedha na kubadili fuko hilo la kuleta uthabiti kuwa shirika la fedha la Ulaya.
Katika mjadala bungeni kiongozi wa wabunge wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Germany AfD, Alice Weidel , alikaripiwa na spika wa bunge la Ujerumani Wolfgang Schaueble kwa kuwabagua wanawake wanaovaa hijabu katika hotuba yake.
Mwandishi: Sekione Kitojo rtre
Mhariri:Gakuba, Daniel