Kansela Merkel akamilisha ziara ya bara la Asia
19 Julai 2010Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekamilisha ziara yake ya wiki moja ambapo ametia saini makubaliano kadha na maafisa wa mataifa ya bara la Asia. Kansela hata hivyo amekamilisha ziara hiyo kwa kuzuru Karakhstan , nchi yenye utajiri mkubwa wa mafuta, akitia saini makubaliano ya kibishara yenye thamani ya zaidi ya euro bilioni 2.
Ujerumani imeanza kujitoa kutoka katika kipindi cha kuporomoka kwa uchumi na kuingia katika kipindi cha ukuaji wa kuridhisha katika miezi michache iliyopita kwa mgongo wa mauzo yake ya nje pamoja na kuongezeka pia kwa maslahi ya kibiashara nchini Urusi, China na hivi sasa Kazakhstan, hali inayoweza kusaidia kuimarisha ukuaji huo.
Makubaliano muhimu yaliyofikiwa jana Jumapili ni mkopo wenye thamani ya euro milioni 100 uliotolewa na Deutsche Bank kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini Kazakhstan.
Rais wa Kazakhstan Nursultan Nazarbayev ameyahimiza makampuni ya Ujerumani kujihusisha zaidi katika taifa hilo, wakati alipokutana na kansela Merkel. Kansela Merkel amedokeza kuwa makampuni ya Ujerumani yanapenda kujishughulisha zaidi na masuala ya matumizi ya nishati, mawasiliano ya simu, ujenzi, utengenezaji bidhaa na kilimo.
Ameongeza kuwa masharti muhimu kwa kampuni hizo kujishughulisha zaidi nchini Kazakhstan ni pamoja na hali jumla ya kuaminika na msingi imara kwa ajili ya kuaminiana.
Kansela Angela Merkel aliondoka katika jimbo la Shaanxi asubuhi jana Jumapili, akikamilisha ziara ya siku nne nchini China ambapo alikutana na viongozi wa serikali pamoja na wa biashara na kutia saini makubaliano kuhusu biashara, nishati na mazingira.
Katika mji mkuu wa jimbo la Xi'an , Merkel alifuatana na waziri mkuu Wen Jiabao katika ziara ya ukaguzi wa makampuni ya Ujerumani na China, ikiwa ni pamoja na miradi ya pamoja inayotekelezwa na kampuni la Ujerumani la Siemens.
Merkel amesema kuwa kiwanda hicho cha Siemens ni ishara ya uhusiano mzuri baina ya nchi hizo mbili, pamoja na matarajio mazuri ya hapo baadaye.
Hata hivyo, katika mkutano wa hapo kabla wakiwa na Merkel na Wen, viongozi wa makampuni ya Ujerumani na China walikosoa utaratibu wa masoko katika kila nchi.
Wakati huo huo kansela wa Ujerumani Angela Merkel amempoteza mshirika muhimu katika majimbo jana Jumapili, ambapo meya wa jiji la Hamburg kutoka chama chake cha CDU , Ole von Beust, alitangaza kujiuzulu.
Ni waziri mkuu wa sita kutoka chama cha CDU kujiuzulu katika muda wa miezi 12, na kupunguza jumla ya viongozi waandamizi katika chama hicho kikubwa nchini Ujerumani. Pamoja nao ni kujiuzulu pia kwa rais wa Ujerumani Horst Koehler ambaye alijiuzulu ghafla Mei mwaka huu.
Beust alitangaza kujiuzulu saa chache baada ya kushindwa vibaya kwa sera zake za elimu katika jimbo la Hamburg ambapo kulifanyika kura ya kwanza ya maoni juu ya suala hilo.
Zaidi ya wapiga kura asilimia 54 waliikataa sera ya mipango ya serikali ya jimbo hilo kubadilisha mfumo wa shule za umma ambapo watoto watatumia miaka sita badala ya minne kwa masomo ya shule za msingi.
Mwandishi : Sekione Kitojo / DPAE
Mhariri: Josephat Charo