Kansela Gerhard Schröder atetea umuhimu wa kuondolewa China vikwazo
15 Aprili 2005Berlin
Kansela Gerhard Schröder,akihutubia katika bunge la shirikisho mjini Berlin,ametetea kwa mara nyengine tena haja ya kuondolewa vikwazo vya silaha dhidi ya jamhuri ya umma wa China.Kansela Gerhard Schröder anasema vikwazo hivyo vilivyowekwa tangu miaka 15 iliyopita,kufuatia mauwaji katika uwanja wa Tiananmen,vinastahiki kubatilishwa .Kansela Gerhard Schröder amesisitiza kwamba msimamo wake huo haujashawishiwa na tamaa ya kuipatia China silaha za Ujerumani.Waziri wa mambo ya nchi za nje Joschka Fischer amezungumzia umuhimu wa China kiuchumi na kwa hali ya utulivu ulimwenguni.Hata hivyo ameitaka jamhuri ya umma wa China iidhinishe kwanza waraka wa umoja wa mataifa kuhusu haki za binaadam,na kusaka ufumbuzi wa amani katika mzozo pamoja na Taiwan kabla ya vikwazo hivyo vya silaha kuondolewa.Mwenyekiti wa chama cha walinzi wa mazingira Die Grüne,bibi Claudia Roth anapinga kuondolewa vikwazo hivyo kwasababu,anasema China inavunja haki za binaadam.Wabunge wa vyama ndugu vya CDU/CSU na wale wa kiliberali wa FDP wana msimamo sawa na huo.