1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Angela Merkel akamilisha ziara yake barani Afrika

Oumilkheir Hamidou
31 Agosti 2018

Kansela Angela Merkel anamaliza ziara yake ya siku kataika nchi tatu za Afrika nchini Nigeria. Lengo la ziara hiyo ni kushadidia umuhimu wa ushirikiano wa kiuchumi na kusaka njia za kupambana na uhamiaji haramu

https://p.dw.com/p/3472z
Nigeria Besuch der Kanzlerin Merkel
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

 

Kansela Merkel amepokelewa kwa hishma za kijeshi na mwenyeji wake, rais wa Nigeria Muhammadu Buhari alipowasili mjini Abuja. Kansela Merkel amesifu umuhimu wa kiuchumi wa taifa hilo la Afrika magharibi na kumsihi rais Buhari ahakikishe uchaguzi unaokuja wa rais unakuwa huru na wa haki.

"Nigeria ni mojawapo ya mataifa muhimu barani Afrika" amesema kansela Merkel. Koloni hilo la zamani la Uingereza lenye wakaazi milioni 190  ni mshirika wa pili mkubwa wa kiuchumi wa Ujerumani katika kanda ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.

 Kansela amesifu pia mchango wa Nigeria, katika kulinda hali ya utulivu katika eneo hilo. Serikali kuu ya Ujerumani inafuatilizia kwa makini maendeleo ya kiuchumi na kisiasa ya Nigeria ambayo ndio kwanza imeanza kujikwamua toka mzozo mkubwa wa kiuchumi.

Kansela Merkel na rais Buhari mjini Abuja
Kansela Merkel na rais Buhari mjini AbujaPicha: DW/U. Musa

Ujerumani kupanua ushirikiano wa kiuchumi na Nigeria

Kansela Angela Merkel ameahidi ushirikiano wa kiuchumi pamoja na Nigeria utapanuliwa na kuingiza pia sekta ya kilimo. Pembezoni mwa ziara ya kansela Merkel mjini Abuja, mikataba mitatu  ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Nigeria imetiwa saini.

"Hali ya utulivu na utawala bora ndio masharti muhimu yanayotanagulizwa mbele na makampuni ya Ujerumani" amesema kansela Merkel. Kuhusu uchaguzi wa rais uliopangwa kuitishwa Februari mwakani kansela Merkel amesisitiza tunanukuu"Vijana watajeresha imani kwa nchi yao ikiwa hali ya uwazi itatawala, ikiwa rushwa itapigwa vita na kama uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

Wakimbizi kutoka mataifa kadhaa ya Afrika yakiwemo Nigeria,Ghana na Senegal wameokolewa na kikosi cha ulinzi wa mipaka cha Umoja wa ulaya Frontex
Wakimbizi kutoka mataifa kadhaa ya Afrika yakiwemo Nigeria, Ghana na Senegal wameokolewa na kikosi cha ulinzi wa mipaka cha Umoja wa ulaya FrontexPicha: Imago

Juhudi za kupambana na wahamiaji kinyume na sheria

Mwishoni mwa ziara yake ya siku tatu katika nchi tatu za Afrika kansela Merkel amezungumza na waandishi habari mjini Abuja na kuelezea matokeo ya ziara hiyo:

"Katika kila nchi kati ya hizo tatu, viongozi wana mtazamo bayana kuhusu mustakbal wa nchi yao. Hilo limedhihirika kutokana na mazungumzo tuliyokuwa nayo, kila mmoja ana matarajio yake kuhusu sekta gani kuendeleza ushirikiano. Wote ni washirika imara naiwe Senegal, Ghana au Nigeria .Na wote wanataka kuendeleza biashara kwa hivyo tunashindana kibiashara na mataifa mengine."

Sawa na alivyotamka nchini Senegal na Ghana, mjini Abuja pia kansela Merkel amezungumzia uwezekano wa kurahisisha njia za uhamiaji halali kwa wanafunzi kupatiwa msaada wa kuja kupata mafunzo nchini Ujerumani. Amekumbusha wanafunzi 1200 wa Nigeria wanasoma wakati huu tulio nao nchini Ujerumani.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga