KANO:Ajali ya moto yauwa watu 70
28 Machi 2007Watu 70 wameuawa na wengine 20 kujeruhiwa baada ya moto kuwaka pale lori la mafuta liliposhika moto katika eneo la kaskazini la Nigeria.Majeruhi hao wanaendelea kupata matibabu baada ya moto huo kutokea kwenye barabara moja kwenye jimbo la Kaduna kwa mujibu wa msemaji wa polisi katika eneo hilo.
Lori hilo lililokuwa limebeba lita alfu 33 za mafuta lilipinduka mahali ambapo barabara ilipinda.Wapita njia walipuuza onyo la msemaji huyo la kutokinga mafuta yaliyokuwa yakitiririka ndipo walipoteketea.Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.
Nchi ya Nigeria ni mzalishaji mkubwa wa mafuta machafu barani Afrika lakini sekta hiyo inakabiliwa na vitendo vya rushwa na uongozi mbaya unaosababisha uhaba wa mafuta ya kupikia vilevile petroli.Mwaka jana katika mji wa Lagos,bomba la mafuta lililopasuka lilishika moto mwezi Disemba na kusababisha vifo vya watu 265.