Kanisa la Pützchen mjini Bonn latimiza miaka 100
7 Mei 2007Kulikuwa na shamrashamra katika kanisa la Mtakatifu Adelheid katika kitongoji cha Pützchen hapa Bonn. Katika warsha iliyokuwa na mada ´Pützchen grüßt die Welt,´ yaani kanisa la Putzchen laisalimia dunia, watoto wa shule ya Bonn Beul walijitokeza kusherehekea miaka 100 ya kanisa la Pützchen. Kundi la wacheza ngoma kutoka nchini Bolivia nalo halikuwachwa nyuma katika tafrija hiyo.
Wilhelm Wester ni mwenyekiti wa kamati ya kanisa la Pützchen. Binafsi ameridhishwa na jinsi sherehe zilivyofanyika.
´Ilikuwa siku nzuri sana. Ni siku ambayo imedhihirisha umuhimu wa kanisa la kikatoliki duniani. Tumeweza kueleza juu ya miradi mingi ya masharika ya kikanisa, kimataifa na hata shule ambayo yanadhamini miradi yake katika sehemu mbalimbali uliwenguni. Tumeweza pia kuweka wazi kwa watu wote duniani kuwa Wajerumani wa Pützchen wanawajali masilahi yao.´
Bwana Wilhelm Wester alisema kanisa la Pützchen lina mradi wa kuwasaidia wakimbizi katika kambi moja ya wakimbizi nchini Jamahuri ya kidemokrasia ya Kongo. Wakimbizi hupokea chakula na mahitaji mengine lakini lengo hatimaye ni kuwawezesha wajitegemee binafsi katika siku za usoni.
Kanisa hilo pia hudhamini mradi unaoendeshwa na watawa wa kikatoliki nchini Misri. Mradi huo unajumulisha utoaji wa elimu hususan kwa wasichana, utoaji wa huduma za matibabu na kutoa mafunzo ya dini ya kikristo.
Pützchen ni mahali ambapo zamani za kale palikuwa na kisima cha maji kilichochimbwa na Adelheid. Bwana huyo hakuwasaidiwa watu na wanyama waliokuwa wakikabiliwa na ukosefu mkubwa wa maji kutokana na ukame mkali bali pia kuanzisha mahali ambapo watu kutoka sehemu mbalimbali duniani huja kuhiji.
Katika kisima cha Adelheid misheni hii ilianzia kuwa kanisa huru mnamo mwaka wa 1906. Mwaka jana wa 2006 kanisa la Pützchen lilitimiza miaka 100, lakini maadhimisho yakapangwa kufanyika Jumapili tarehe 6 mwezi Mei mwaka huu.
Tangu kuanza kwa safari za hija katika kanisa la Pützchen idadi kubwa ya watu wamekuwa wakizuru mahala hapa licha ya shughuli nyingi za kila siku. Nyakati za sasa watu wengi wanakabiliwa na matatizo mazito ya ukosefu wa maji safi ya kunywa, magonjwa na vifo vinavyotokana na vita na machafuko katika sehemu mbalimbali duniani.
Bwana Wilhelm alisema changamoto nyengine kubwa zinazowakabili binadamu duniani kote ni utapiamlo, ukosefu wa elimu na janga la ukimwi.
Mwenyekiti wa kamati ya kanisa la Pützchen bwana Wilhelm Wester, anasema kuna dalili nzuri za watu wengi zaidi kujitokeza kuwasaidia watu wengine duniani.
´Cha kufurahisha tunachokiona ni kwamba watu wanajitokeza kwa wingi zaidi ili kuwaonyesha watu kipi kinachowezekana na kuwashawishi wafanye mengi zaidi katika siku za usoni.´
Bwana Wilhelma alisema kwa sababu kanisa la Pützchen sasa limetimiza miaka 100, kanisa hilo linataka kuwashakikishia washirika wa makanisa ya kiinjili na walimwengu wote kw ajumla kwamba bado wanaweza kuendelea kulitegemea katika maswala ya misaada.