1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanisa Katoliki Ujerumani laomba radhi

25 Septemba 2018

Kanisa Katoliki nchini Ujerumani limewaomba radhi wahanga wa vitendo vya unyanyasaji wa kingono kutoka kwa mapadri, huku Kadinali mwandamizi nchini humo akitaka wahusika wa vitendo hivyo kufikishwa mbele ya sheria.

https://p.dw.com/p/35Tog
Deutsche Bischofskonferenz - Kardinal Reinhard Marx
Picha: picture alliance/dpa/A. Weigel

Mkuu wa taasisi ya maaskofu nchini Ujerumani, ya German Bishops Conference, Kadinali Reinhard Marx amesema amefedheheshwa na vitendo vya unyanyasaji vilivyofanywa kwa miongo kadhaa ambavyo vimepunguza imani na namna ambavyo wengi wamevipuuza vitendo hivyo kwa muda mrefu.

Amenukuliwa akisema "inatakiwa ielezwe wazi kabisa kwamba unyanyasaji wa kingono ni uhalifu. Wale wanaokutwa na hatia ya vitendo hivyo wanatakiwa kuadhibiwa. kwa muda mrefu kanisa limepuuzia vitendo hivyo, kukana, kutetea na halikutaka kukubali ukweli wa vitendo hivyo. Kama mwenyekiti wa taasisi ya maaskofu, ninaomba radhi kwa kushindwa kwetu pamoja na maumivu, na mimi binafsi pia ninaomba radhi".

Matamshi haya ya kufadhaisha yaliyotolewa na Kadinali Marx yamekuja wakati kanisa likichapisha ripoti mbaya inayoonyesha watoto 3,700, wengi wao wakuwa ni wa kiume nchini Ujerumani walinyanyaswa kati ya mwaka 1964 hadi 2014.

Waandishi wa ripoti hiyo hata hivyo wamesema, takwimu hiyo ilikuwa ni ya kidogo tu, na kwamba ukubwa hasa wa tatizo hilo, huenda ukawa ni zaidi ya hapo.

Litauen PBesuch Papst Franziskus
Papa Francis ahofia kwamba kashfa hizo zinaweza kuwafukuza waumini hasa vijana kwenye kanisa hilo.Picha: Reuters/I. Kalnins

Kanisa hili linaomba radhi, katika siku ambayo pia kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Francis akikiri kwamba kashfa ya unyanyasaji wa kingono inayolitikisa Kanisa Katoliki inawafanya waumini wengi sasa kuachana na kanisa hilo. Amesema, ni lazima kanisa libadilishe njia zake iwapo linataka kizazi kijacho kusalia ndani ya kanisa hilo.  

Wahanga wanaikosoa ripoti hiyo kwa mapungufu.

Ripoti ya unyanyasaji wa kingono ndani ya Kanisa Katoliki nchini Ujerumani imefichua kwamba zaidi ya nusu ya wahanga walikuwa chini ya miaka 13 na wengi wao wakiwa ni wavulana. Na kila shauri la sita lililopitiwa lilihusisha ubakaji na angalau mapadri 1,670 walihusishwa. Takribani matukio 969 ya wahanga wa unyanyasaji huo walikuwa ni wavulana waliohudumia altareni.

Kwa wastani, unyanyasaji ulifanyika mara kadhaa, katika kipindi cha angalau miezi 15.

Mkutano wa Maaskofu wa Ujerumani, umechapisha ripoti hii leo, lakini tayari ripoti hiyo ilikuwa imevuja mapema mwezi huu na kwa kiasi kikubwa ilikosolewa kwa kukosekana kwa uwazi na kanisa kukataa kuwapa nyaraka halisi wachunguzi.

Ripoti hiyo iliagizwa na Taasisi hiyo ya Maaskofu na kufanyiwa uchunguzi na wataalamu kutoka chuo kikuu cha Giessen, Heidelberg na Mannheim.

Wachunguzi hao waliandika kwamba kulikuwa na ushahidi kwamba baadhi ya mafaili yaliharibiwa, na mashauri mengi hayakufikishwa mbele ya sheria. Mara nyingine, watuhumiwa wa unyanyasaji, na hususan mapadri, walihamishiwa tu kwenye dayosisi nyingine bila ya waumini kuarifiwa chochote kuhsu historia zao.

Hata hivyo, wahanga wameikosoa ripoti hiyo kwa kutokuwa na kile kilichohitajika ili kuwabaini wahalifu. Wamelitaka kanisa kuleta wachunguzi huru kufanya ukaguzi wa kina, na kuongeza kuwa watatakiwa kulipwa fidia.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/APE.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman