Kanisa Katoliki laitisha maandamano ya amani Kongo
31 Desemba 2017Kabila ambaye waandaaji wa maandamano hayo wanamtaka atamke wazi kuwa hatawania muhula wa tatu wa uongozi, amekuwa madarakani tangu mwaka 2001 wakati aliposhika madaraka ya urais baada ya baba yake Laurent Kabila kuuawa.
Kabila alikataa kujiuzulu bada ya kumalizika kipindi chake cha pili na cha mwisho Desemba 2016 hatua iliyosababisha maandamano pamoja na machafuko.
Tangu kipindi hicho maanadamano yamekuwa yakipigwa marufuku licha ya wakati mwingine waandamanaji kukiuka amri ya serikali na kuendelea na maandamano hali ambayo pia imekuwa ikisababisha umwagaji wa damu.
Hatua ya kanisa Katoliki kuitisha maandamano ya leo Jumapili licha ya serikali kuyazuia yasifanyike inawafanya baadhi ya wachambuzi kuonya juu ya uwezekano wa kukosekana utulivu.
"Maandamano ya leo Jumapili nchini Kongo yanaweza kuwa makubwa zaidi kuliko yale ya mwaka jana" ameandika kupitia ukurasa wa twitter Jason Stearns mchambuzi aliyebobea katika masuala ya siasa za Kongo kutoka chuo kikuu cha New York kinachohusika na mahusiano ya kimataifa.
Anasema vyama vyote vikubwa vya upinzani, asasi za kiraia, makundi ya vijana wanaharakati pamoja na kanisa Katoliki yanaunga mkono maandamano hayo ya leo Jumapili.
Uchaguzi ulipaswa kufanyika mwaka huu
Uchaguzi ulikuwa ufanyike mwishoni mwa mwaka huu chini ya makubaliano yaliyoasimamiwa na kanisa katika juhudi za kuzuia machafuko kwenye taifa hilo kubwa lenye utajiri wa madini ambalo halijawahi kushuhudia mabadilishano ya madaraka kwa njia ya amani tangu lijipazie uhuru wake kutoka Ubeligiji mwaka 1960.
Baada ya kuahilishwa mara kadhaa hasa kutokana na vurugu katika mkoa wa Kasai uchaguzi huo uliocheleweshwa sasa umepangwa kufanyika Desemba 23, mwakani.
Kiasi ya makanisa 150 ya kanisa Katoliki yametoa mwito kwa waumini wao kuitikia wito wa kuandamana leo Jumapili mjini Kinshasa wakiwa na biblia mkononi ili kushinikiza kutekelezwa kwa makubaliano yaliyotiwa saini mwaka mmoja uliopita yaliyokuwa na lengo la kurejesha uthabiti nchini humo ikiwa ni pamoja na kumtaka Kabila kuondoka madarakani.
Si baraza la maaskofu nchini humo au mwakilishi wa serikali ya mjini Vatican amezungumzia lolote kuhusiana na maandamano hayo.
Gavana wa mji huo Andre Kimbuta wenye watu milioni 10 amesema jana Jumamosi kuwa maandamano hayo yasiyo na kibali hayawezi kuendelea kwa maelezo kuwa mji huo hauna maafisa wa polisi wa kutosha kusimamia maandamano ya leo.
Hata hivyo msemaji wa waratibu wa maandamano Leonie Kandolo alisisitiza kuwa licha ya kauli hiyo ya serikali maandamano ya leo yatafanyika na kuwa maafisa wa mji huo pamoja na polisi wanalazimika kutimiza wajibu wao kuwalinda raia na mali zao.
Waandaaji wa maanadamano wametoa mwito kwa waumini kukusanyika baada ya misa ya asubuhi kwa ajili ya kushiriki maandamano leo.
Katiba ya Kongo inamzuia Kabila kuwania muhula wa tatu wa uongozi lakini makubaliano yaliyofikiwa yanamruhusu kusalia madarakani hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika.
Mwandishi: Isaac Gamba/ afpe
Mhariri : Sekione Kitojo